BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu

Kessy akiwa na bibi yake

WACHEZAJI wengi wa Tanzania ndoto zao zimekuwa ni kupata nafasi ya kucheza katika klabu kongwe za Simba na Yanga licha ya kuwa na mizengwe mingi ndani ya timu hizo juu ya Wachezaji wao.

Hassan ' Kessy' Ramadhani  ni beki wa kulia wa klabu ya Simba ambaye alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro baada ya viongozi wa Simba kuvutiwa na kipaji chake.

Kessy aliwahi kuondoka kwenye kambi ya timu yake  kutokana na uongozi wa Simba kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wake ikiwemo kutompatia sehemu ya kuishi, sasa amerejea na anasema amerudi kwa kasi ili kuhakikisha anaimarisha nafasi yake katika kikosi cha kwanza.

BOIPLUS imefanya mahojiano na Kessy ili kujua maisha yake nje ya soka kwavile watu wengi wanafahamu ubora wake akiwa uwanjani, nje ya uwanja mambo yake yapoje?
Mazungumzo kati ya mwandishi wetu na Kessy yalikuwa hivi; 

BOIPLUS: Wewe ni mtu wa aina gani katika maisha ya kawaida ukiwa nje Uwanja?

Kessy: Mimi ni mtu wa kawaida   ninayependa kujichanganya na kila mtu  na sipendi  kujionyesha mbele za watu kuwa nipoje kitendo ambacho sio rahisi kunigundua   kuwa nina fedha wala sina.

BOIPLUS : Kwa nini unapenda kujichanganya na kila mtu wakati wengine wakishapata majina wanachagua marafiki?

Kessy: Napenda sana kukaa na kila mtu haijalishi ni tajiri, masikini, mlevi, mvuta bangi au  hadhi yake ikoje kwa sababu  najua kuna leo na kesho maisha yanabadilika, leo nipo kwenye mpira lakini kesho sipo. 

Endapo  nitasema nijitenge na watu wa mtaani kwangu wakati huu, basi maisha yangu yatakapobadilika watakuja kuniuliza kiko wapi nilichokuwa najivunia, nafikiria  sana maisha ya baadae.

Kessy akiwa na Awadh Juma

BOIPLUS: Licha ya kuwa na marafiki  wa aina tofauti, Je  mtu wako wa karibu zaidi ni nani ambae hata ukipata tatizo anakushauri kwa haraka?

Kessy: Mtu  ninayekuwanae karibu sana hata hiki kipindi kile cha matatizo  na timu yangu ni 'Baby wangu'  namaanisha  mchumba wangu kwa  sababu  ananifariji sana ninapokuwa na tatizo lolote ila siwezi kumtaja jina kwa sasa  siku ikifika nitamuweka wazi.

BOIPLUS : Hutaki kumtaja jina sawa, Je  yupo Morogoro au Dar es Salaam?

Kessy: Yeye anaishi Dar es Salaam na kipindi ninachohitaji kuwa nae nikiwa sijabanwa na kazi   ndio tunakutana lakini kila siku tunawasiliana kwa simu.

BOIPLUS : Ni kitu gani kinaweza kukufanya uwe mwenye hasira au furaha?

Kessy: Nakasirika sana endapo mtu atanichukulia mimi kama mtu  mhuni wakati sina tabia hiyo lakini pia nikisemwa vibaya . Anaenifanya niwe na furaha ni mpenzi wangu kwavile nampenda sana na kuna vitu ananiambia vinanifurahisha. 

BOIPLUS : Unapendelea kula chakula gani?

Kessy: Napenda sana kula ugali wa muhogo na mlenda, wali samaki  au nyama. Asubuhi napendelea kunywa uji wa ulezi  halafu baadae chai.

BOIPLUS : Ugali wa muhogo  una mapishi yake na sio rahisi,  nani anakupikia au mwenyewe unaweza?

Kessy: Mama ndio anapenda kunipikia ugali wa muhogo nikiwa Dar es Salaam. Sio kama sijui kupika ila mama anapenda kuniona nakula na kupumzika lakini nikiwa Morogoro kwa bibi napika mwenyewe.

BOIPLUS: Kinywaji na tunda gani unapendelea?

Kessy: Napenda kunywa Bavaria kwa kuwa haina kilevi, tunda ninalopenda ni ‘Apple’.

BOIPLUS : Tofauti na kupika, kazi gani nyingine za nyumbani  unajua kuzifanya?

Kessy: Kazi zote naweza kufanya, nikiwa kwa bibi yangu binti Ramadhani  ndio nafurahia kufanya kazi, huwa namsaidia kila kitu cha  nyumbani kama kufua, kuosha vyombo   hadi kukuna nazi akiwa anapika yeye.

BOIPLUS: Siku yako haiwezi kupita bila kufanya nini?

Kessy: Siwezi kupitisha siku bila kucheza ‘Game' za mpira kwenye Play Station au kuchati kwenye mitandao ya kijamii hasa nikiwa na mawazo. Ingawa napenda pia kuogelea ila sio kila siku.BOIPLUS: Unapenda kuwa na muonekano gani kuanzia kimavazi na mtindo wa nywele?

Kessy: Napenda mavazi ‘Simple’ naweza kuvaa pensi, T-shirt na miguuni navaa viatu vitakavyoniweka huru popote. Kwa upande wa Nywele sina mtindo mmoja siku nyingine kipara, kiduku au naziacha kidogo.

BOIPLUS : Rangi gani inakuvutia?

Kessy : Navutiwa na rangi nyeupe na aliyenifanya niipende zaidi ni mpenzi wangu.

Post a Comment

 
Top