BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar

MKUU wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga Jerry Muro amesema ataendelea kuwaita watani wao wa jadi Simba jina la 'wamatopeni' mpaka hapo watakaposhiriki michuano ya kimataifa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya baadhi ya mashabiki wa Simba kutaka kwenda kumshitaki Afisa habari huyo kwa Waziri wa habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye baada ya malalamiko yao ya muda mrefu kutofanyiwa kazi na Shirikisho la mpira wa miguu TFF huku Jerry mwenyewe akitamba kuwa hawamtishi.

"Naona mashabiki hao wamesahau mwaka 1992 walivyomvalisha mbwa jezi ya mchezaji wetu baada ya kututoa kwenye michuano ya mapinduzi na hata miaka ya karibuni walivyokuwa wanatufunga kwenye mabonanza ya Mtani Jembe walikuwa wanachonga sana sasa ni wakati wao wa kutulia na sitoacha kuwaita wa matopeni," alisema Muro.

Katika siku za karibuni Muro amekuwa akitupiana maneno na Afisa habari wa Simba Haji Manara mpaka ikafikia kushitakiwa kwenye kamati ya maadili ya TFF lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.

Wiki iliyopita  Manara alisema mbele ya vyombo vya habari kuhusu kutocheza mechi za ligi hadi viporo vya Yanga na Azam vimalizike huku Jerry nae akisema Simba wanatakiwa wakae kimya kwakua hawashiriki michuano ya kimataifa.

Mashabiki wa mpira hapa nchini wamekuwa wakikosoa maneno ya wasemaji hao ambayo wakati mwingine yanakuwa sio ya kimichezo. BOIPLUS iliwahi kuandika makala kuelezea jinsi wasemaji hao wanavyotumia ofisi zao kwa habari zao binafsi badala ya kuongelea maendeleo ya timu zao.

Post a Comment

 
Top