BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Kigali


TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam ilimaliza mazoezi ya jana  jioni na kurejea kwenye hoteli tulivu ya The Mirror iliyopo mitaa Remera Kisementi hapa Kigali kwa ajili ya kupumzika na kusubiri kipute cha klabu bingwa Afrika dhidi ya APR, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Amahoro leo saa 9:30 alasiri ambayo ni sawa na saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Wachezaji wote wa Yanga ambayo iliwasili hapa juzi mchana, wapo 'kamili gado' kwa ajili mchezo huo isipokuwa Amissi Tambwe ambaye katika mazoezi ya jana alionekana akifanya peke yake kufuatia maumivu aliyopata katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya African sports. Hata hivyo kocha wa timu hiyo Hans Van Pluijm amesema anaweza kumtumia mchezaji huyo.


MZUKA UKOJE?
Wachezaji wa Yanga wameonekana kuwa wenye kujiamini sana licha ya ugumu wa mechi hii ambao kila mmoja anaujua, bila shaka mbinu za mholanzi Pluijm ndizo zinazowapa kiburi. Mashabiki takribani 35 waliokuja kuishangilia timu hiyo pamoja na watanzania wanaoishi huku ndio watakaowapa morali mabingwa hawa wa soka Tanzania Bara ili kupata matokeo mazuri. 

WANAKUTANA NA APR GANI?
Ukiijua historia ya APR na kiwango walichonacho kwa siku za hivi karibuni huwezi kuiita mechi hii rahisi. Ni mechi ngumu ambayo itakuwa na mvuto wa aina yake. APR inayotumia vijana wa nyumbani tu tena wengi wakitokea kwenye Academy yao iliyopo hapa Kigali, wametoka kuiondosha Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 4-2 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi ya mabingwa Afrika.

Mbali na matokeo hayo, Wanajeshi hao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya Rwanda wakiwa na pointi 30 huku Mukura Victory Sports wakiongoza kwa pointi 32. Yanga pia iko nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Vodacom nyuma ya mahasimu wao Simba. Ushindi wa mabao 3-0 walioupata APR ugenini dhidi ya Musanze FC nao umewafanya wawe na morali zaidi.

YANGA WATALIPA KISASI CHA MWAKA 1996?
Siku hazigandi, na kama ziliganda basi zimeyeyuka. Yanga wamepata nafasi ya kurudisha kisasi cha kuondolewa mashindano na APR walipokutana kwa mara ya mwisho kwenye michuano hii mwaka 1996 pale ilipofungwa bao 1-0 Kigali na kisha kufungwa 3-1 jijini Dar es Salaam. Yanga hii ya sasa inao uwezo wa kurudisha kisasi kutokana na ubora wa kikosi ambao mashabiki wao hukiita 'Cha Kimataifa'. 

KOCHA APR ANA WIKI MOJA TU
APR imempa mkataba wa miezi sita kocha mkongwe raia wa Tunisia, Nizar Khanfir ambaye ametua jumamosi iliyopita akitokea Stade Gabèsien FC


Mchezo wa kwanza kwa kocha huyo ambaye aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Tunisia (U23) utakuwa dhidi ya Yanga. Kabla ya kutua kwa kocha huyo, APR ilikuwa chini ya Emmanuel Rubona ambaye sasa anakuwa msaidizi wa Nizar. Je, Yanga itamkaribisha kwa kichapo?, muda utatoa majibu.

YANGA WATAZAMENI WACHEZAJI HAWA KWA JICHO LA TATU
Wakiwa nyumbani, APR watataka kupata ushindi mnono ili kujirahisishia kazi watakapokwenda Tanzania kwenye mchezo wa marejeano. Lakini lengo kuu la Yanga ni kupata ushindi na ikishindikana basi ipate japo sare. 


Kampeni hii ya APR inawategemea zaidi washambuliaji wao wanaoongozwa na Abdul Rwatubyaye ambaye katika mchezo uliopita dhidi ya Mbabane Swallows, aliifungia APR mabao yote matatu. Kuna mshambuliaji mwingine, Djihad Bizimana ambaye pia anaweza kuiletea madhara safu ya ulinzi ya Yanga.

Lakini pia APR inajivunia mlinzi wake wa kati, Emery Bayisenge ambaye ni 'mchawi' wa mipira ya adhabu. Jumatatu iliyopita Bayisenge aliipatia ushindi  wa mabao 3-0 timu yake katika mchezo wa ligi kuu kwa kufunga mara mbili kwa mipira ya adhabu.

Kuepukana na madhara ya Bayisenge, Yanga watapaswa kucheza kwa tahadhari sana hasa kwenye eneo lao la 18 ili kukwepa kucheza faulo zisizo za lazima.

MASHABIKI APR NA RAYON SPORTS KAMA SIMBA NA YANGA TU
Ukiwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Simba au Yanga ikawa inacheza mchezo wa kimataifa, basi unaweza usifahamu kirahisi ipi ni timu ngeni na ipi mwenyeji kwavile zote zinakuwa na mashabiki tena wengi tu. 

BOIPLUS ilitaka kujua hali ikoje hapa Kigali hasa kwa mashabiki wa Rayon Sports ambao ni wapinzani wakubwa wa APR. Jibu ni kwamba asilimia kubwa ya mashabiki wa Rayon wamejiandaa kuishabikia Yanga ipate ushindi dhidi ya mahasimu wao APR. 'Support' yao ilianza kuonekana jana kwenye mazoezi ya Yanga asubuhi kwa mashabiki hao kujaa uwanjani kama vile kulikuwa na mechi.

KILA KONA NI NIYONZIMA TU
Tuache masihara, Haruna Niyonzima anapendwa jamani. Dalili za wanyarwanda kumkubali kiungo huyo mwenye mbwembwe nyingi uwanjani zilianza kuonekana mara baada ya kuvuka mpaka pale Rusumo ambapo mashabiki wengi walianza kugombea kununua jezi yake.

Hapa Kigali baadhi ya mashabiki wa soka waliokiri kuwa ni wa APR walisema kwa leo itabidi waishangilie Yanga ili kuonyesha mapenzi yao kwa Niyonzima.

YANGA ITAPATA MATOKEO MAZURI KUPITIA HAPA
1. Kocha Mpya
Kocha mpya wa APR, Nizar amekiri kuwa ameikuta timu hiyo inacheza vizuri lakini si katika mtindo anaoupenda. Sasa kama amejaribu kuingiza mtindo wake mpya kwa wachezaji ndani ya hizi siku sita alizokaa na timu hiyo basi hiyo ni bahati nasibu ambayo kama haitaangukia upande wake basi ni 'kitonga' kwa Yanga.

Ni ngumu kwa wachezaji wa APR kuzikamata mbinu zote za kocha mpya kwa haraka hivyo, hii ni tofauti na Yanga ambao wamekaa na kocha wao kwa kipindi kirefu.

Kuanzia Ugenini
Kuna faida zake kuanza hizi mechi za mtoano kwa kucheza mechi ya kwanza ugenini. Hii inasaidia kujiandaa kucheza mchezo wa pili nyumbani huku ukiwa unajua unahitaji matokeo ya aina gani kutegemeana na matokeo ya mchezo wa awali.


BOIPLUS itakuletea kila kinachojiri. Tembelea pia kurasa zetu za:
Instagram: @boiplus_blogspot
Facebok: Boiplus Blogspot
Twitter: @BoiplusBlogspot

Kila la heri Yanga
Post a Comment

 
Top