BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Chamazi


TIMU ya soka ya Azam Fc imetinga raundi ya pili ya kombe la Shirikisho CAF baada ya kuifunga Bidvest mabao 4-3 katika mchezo uliochezwa leo kwenye uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Bidvest walikianza kipindi cha kwanza kwa kulishambulia mfululizo lango la Azam lakini washambuliaji wake walioongozwa na winga Maliele Pule walishindwa kuifungia bao timu hiyo.

Dakika ya 23, Ramadhani Singano 'Messi' alikimbia na mpira kwa kasi kabla hajaachia krosi iliyotua kichwani mwa Kipre Tchetche na kuifungia Azam bao la kwanza. Dakika chache baadae Pule aligongana na Aggrey Moris wakiwa katika harakati za kuwania mpira na ikapelekea winga huyo kukimbizwa hospitali kwa matibabu.

Tchetche ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa Bidvest, alipanda kwa kasi na kupiga krosi ambayo ilimaliziwa nyavuni na John Bocco. Wakati Azam wakiwa hawajamaliza kusherehekea bao hilo, mshambuliaji aliyeingia kuchukua nafasi ya Pule, Jabulani Shongwe aliifungia Bidvest bao la kwanza katika dakika ya 43.

Karamu ya mabao katika uwanja wa Chamazi iliendelea wakati Tchetche alipofanikiwa kutegua mtego wa kuotea uliowekwa na walinzi wa Bidvest kisha akampiga chenga kipa Jethren Barr na kufunga bao la tatu kwenye dakika ya 54 kabla Koiekantse Mosiatlhaga  hajawafungia bao la pili 'wasauzi' hao. 

Tchetche alifunga bao lake la tatu na la nne kwa Azam katika dakika 87 baada ya kuwatoka walinzi wa Bidvest na kuachia shuti kali. Wakati mpira watazamaji wakianza kuinuka vitini, Henrico Botes aliipatia Bidvest bao tatu.

Azam imesonga mbele kwa jumla ya mabao 7-3 na sasa itapambana na Esperance ya Tunisia ambayo imeitoa Renaissance kwa jumla ya mabao 7-0

Post a Comment

 
Top