BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga

TIMU ya Tanzania Prisons imeondoka alfajiri ya leo kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya mchezo wake wa ligi kuu dhidi ya African Sports. Mechi hiyo itapigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani siku ya jumapili.

BOIPLUS ilihudhuria mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye uwanja wa chuo cha Magereza Ukonga na kushuhudia kocha mkuu wa timu hiyo Salum Mayanga akiwa mkali muda wote wa mazoezi huku kila mara akilalamikia kitendo cha wachezaji hao kuruhusu bao kwenye dakika za mwisho za mchezo wao dhidi ya Simba.

Katika mazoezi hayo Mayanga alionekana kuwasisitizia wachezaji wake kuhusu nidhamu ya ukabaji ambapo mara kadhaa alisikika akiwakaripia walinzi na viungo wake pale walipochelewa kuwafikia washambuliaji.

Baada ya mazoezi hayo Mayanga alisema ameamua kuongeza nguvu katika eneo hilo kwavile ndilo limewasababishia kupoteza mchezo wao dhidi ya Simba.

Mayanga akitoa maelekezo kwa wachezaji wake

"Mpira ni mchezo wa makosa lakini hatupaswi kujiandaa kukosea, ni lazima tufanye kazi kupunguza makosa, juzi (jumapili) huyu Jumanne (Elfadhili) alijitahidi kucheza kwa maelekezo yangu na kuwazuia Ibrahim Ajib na Hamis Kiiza wasifunge mabao kama alilofunga Awadh Juma

"Lakini akafanya kosa moja la kumuacha Awadh apige mpira bila kumsumbua, akafunga tukapoteza mchezo. " alisema Mayanga kwa masikitiko.

Mayanga alisema kwenye kila mechi huwa anateua mchezaji mmoja na kumpangia jukumu la kuhakikisha hakuna mchezaji wa timu pinzani anapata nafasi ya kupiga mpira moja kwa moja langoni mwao bila kuharibiwa mpango huo.

Post a Comment

 
Top