BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar

Jerry Muro kushoto akiwa na Haji Manara

HAKUNA namna unaweza kuliongelea soka la Tanzania na usizitaje klabu kongwe za Simba na Yanga, hizi ni kama alama si tu kutokana na umri wake bali pia kutokana na mafanikio. Katika hali ya kawaida, klabu hizi zilipaswa kuwa kioo cha klabu zingine changa lakini kwa bahati mbaya hali iko tofauti sana.

Hakuna asiyefahamu kuwa mpira wa miguu ni biashara kubwa sana iliyowafanya watoto wa masikini waendeshe magari ya kifahari na kuishi kwenye mahekalu, ila hii ni biashara kwa wanaojua biashara tu, si kila mtu. Kuna msemo wa kiswahili unasema 'Biashara matangazo', na naamini hii ndio sababu Simba na Yanga ziliamua kuanzisha idara za habari na mahusiano/mawasiliano ili kuwe na watu ambao shughuli yao kubwa ni kutangaza klabu.

Idara hizi kama zingetumika vizuri ndizo zingeweza kuwa chanzo cha mafanikio ya kibiashara kwa timu hizi kongwe. Lakini kiuhalisia hadi sasa Simba na Yanga hazijanufaika na uwepo wake na wa kulaumiwa hapa ni wakuu wa idara hizo ambao ni Haji Manara (Simba) na Jerry Muro (Yanga).Katika siku za hivi karibuni, Manara na Muro wamefanikiwa kuzigeuza idara hizi kuwa ni za habari na mahusiano yao binafsi badala ya klabu. Mara nyingi wanapozungumza na vyombo vya habari wamekuwa wakitumia muda mwingi kurushiana vijembe na kujisifu hasa katika mambo yao binafsi na pale wanapozungumzia timu basi ni majigambo tupu kama vile timu  hizo hazina shida wala mapungufu yoyote.

Maisha ya kujisifu yanawafanya watu walio nje ya timu hizi na ambao wakati mwingine ni wanaoweza kutoa misaada mikubwa tu wasijue timu zina nini na zinakosa nini. Kama kila ukiamka asubuhi unamwambia mkeo kwa sauti ya juu "nikaangie mayai na soseji" ili tu majirani wasikie, wakati ukweli ni kwamba hata uhakika wa mlo mmoja haupo, basi utalala njaa kila siku wakati labda wapo wenye uwezo wa kukusidia.

Leo nimeitazama picha ya makocha wa Yanga na APR walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mchezo wa kesho, unaweza usielewe kuwa hii mechi ni ya Ligi kuu ya Vodacom, ya timu ya Taifa au klabu bingwa Afrika?, kuna tangazo la Star TV, NHIF, Vodacom, Azam TV, Airtel, Startimes na Kilimanjaro. Je hawa wote ni wadhamini wa Yanga?, kama sio kwanini watangazwe pale.

Kocha wa APR Nizar Khanfir katikati na Hans Pluijm wa Yanga wakizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wao wa kesho

Hii ni mechi ya klabu bingwa Afrika na mdhamini wa Yanga (Kilimanjaro) ndiye pekee alipaswa kunufaika kibiashara kwa kuwekwa bango lake kubwa pale nyuma. Ni kweli Kilimanjaro wenyewe wamezubaa hapa lakini kwavile mimi leo nipo na rafiki zangu Manara na Muro, basi niseme tu kwenye hili Muro kachemsha. Haya ndio mambo ya kuyafikiria wakati unaandaa mkutano wa waandishi wa habari. Kama Muro angewaambia Kilimanjaro wamuandalie bango kwa ajili ya 'Press' basi wadhamini hao wangefarijika sana na kibiashara hizi ndizo sehemu unazoweza kuzitumia kumbana mdhamini aongeze pesa kwenye mkataba ujao.

Manara na Muro hawapaswi kuuhamishia mdomoni huu mpira wa Simba na Yanga, ni kuzipoteza timu hizi. Upinzani unapaswa kubaki uwanjani na kwenye mambo ya maendeleo. Sio kwavile wanajua wakisema tu kuna mkutano wa waandishi wa habari basi waandishi wote tutajazana ndio wajisahau na kuamini jambo pekee tunalolifuata ni vijembe vyao, la hasha, tunatamani kusikia mipango ya maendeleo.

Wakati natafakari haya nilijaribu kuzungumza na watu kadhaa ambao ni wanazi wakubwa wa timu mbalimbali barani Ulaya kama vile Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Liverpool, Arsenal, Chelsea, Bayern Munich na nyinginezo nikiwauliza kama wanawafahamu maafisa habari ama wasemaji wa klabu hizo, wachache wanawafamu kwa majina tu na wengi hawawafahamu kabisa. Nikawauliza lini mara ya mwisho waliwaona wakizungumza na vyombo vya habari na waliongea nini, sikupata majibu. Yawezekana hawa watu watakuwa wanafanya kazi zaidi kwenye tovuti za klabu pamoja na kurasa rasmi za mitandao ya kijamii.

Hapa nikafanikiwa kugundua kuwa Manara na Muro wana mambo mengi sana ya kufanya katika kutoa habari na kuimarisha mahusiano  kati ya timu zao na umma wa watanzania na dunia kwa ujumla, na si hii wanayoifanya ya kutambiana tu. Wanapaswa kutafakari haya na kuyafanyia kazi vinginevyo baada ya muda mfupi tutaona timu kama Mbeya City ikikaa vizuri zaidi sokoni kuliko Yanga na Simba zenye mtaji mkubwa wa wapenzi na wanachama. 


Picha ya bango la Mbeya City linalotumika kwenye mikutano na waandishi wa habari

Msemaji wa City, Dismas Ten ni mbunifu sana, kila mara amekuwa akiibuka na jambo jipya kuashiria amepania kuona anatumia vema kiti chake kuitangaza timu hiyo changa. Nikirudi kwa hawa wakongwe, hadi leo hii tovuti ya Yanga ni kizungumkuti, naamini Muro ana uwezo mkubwa tu wa kuhakikisha anaifanya iwe chanzo kikuu cha habari za klabu hiyo, ila kwanini hafanyi hivyo?. 

Kwa upande wa Simba, tayari kampuni ya EAG inaendesha tovuti yao na ina taarifa muhimu kila mara, lakini naamini Manara anapaswa kuwa karibu zaidi na hawa waendeshaji ili kutoa ushauri na kuweka ubunifu wake kila mara. Hivi ndivyo vitu vitawafanya  wawe 'busy' na kusahau habari ya kujisifu "mimi mtoto wa mjini",  "mimi nimesoma sana".

Kwa maoni;
Mobile: 0788334467
E-mail: boiplus.blogspot@boi.co.tz

Post a Comment

 
Top