BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Chamazi
KOCHA mzoefu Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' amesema Azam wana haki ya kufurahia matokeo mazuri yanayoletwa na mabeki wa pembeni hasa Shomari Kapombe lakini wakikutana na timu yenye mawinga 'viberenge' watapata shida.

Akizungumza na BOIPLUS baada ya mchezo wa kombe la FA kati ya Azam na Prisons, Mwaisabula alisema mfumo wanaoutumia Azam wa kushambulia kupitia mabeki wa pembeni ni mzuri kwavile unawapa ushindi, lakini una madhara makubwa ikitokea wakakutana na timu yenye mawinga wenye kasi.

"Azam wameshinda kwavile wachezaji wamefuata vizuri maelekezo ya mwalimu hasa kuhusu mfumo wanaoutumia, lakini kwa mawinga ninaowajua mimi kama wa enzi zile akina Edibily Lunyamila, Steven Mapunda na wengineo, hawa Azam wangekuwa wanalia sana.

"Hata watakapopambana na Esperance ni lazima wawe makini sana na huu mfumo, wale waarabu ni wajanja na wana kasi." alisema Mwaisabula

Kwa upande wake kocha wa Azam, muingereza Stewart Hall alipoulizwa juu ya athari za mfumo huo alikiri kuwa ni hatari na uliwadhuru kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Bidvest Wits.

"Ni kweli unatusaidia lakini wakati mwingine unatuletea shida, kama ulitazama Bidvest walitufunga kwa style hiyo. Kapombe akipanda mara mbili mfululizo halafu ikatokea tukashambuliwa ghafla basi nahitaji kumpatia Bodaboda, " alisema Hall huku akicheka.

Azam wamefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya FA baada ya kuifunga Prisons mabao 3-1 

Post a Comment

 
Top