BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
MATOKEO mabaya ambayo Mbeya City wameyapata kwenye mechi zao zilizopita yamekuwa yakiwaumiza mashabiki wengi wa timu hiyo miongoni mwao ni mshambuliaji wao wa zamani Mwagane Yeya.

Yeya ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji nyota walioiwezesha Mbeya City kufanya vizuri msimu wao wa kwanza na kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu, amewaambia wachezaji wa City kwamba ni lazima wapambane kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi.

Alisema ni jambo la aibu mchezaji kuishusha daraja timu hivyo wanapaswa kuweka malengo kwenye mechi zao zilizobaki huku akiamini kwamba hiki ni kipindi cha mpito kwao.

"Kikubwa ni kujiwekea malengo nakumbuka huu ni msimu wa pili kwa Mbeya City kufanya vibaya ila naamini ni kipindi cha mpito, wachezaji wanapaswa kuweka uzalendo mbele kama tulivyofanya msimu wa kwanza.

"Haya matokeo siyo mazuri huwa yanaumiza ila bado wana nafasi ya kupambana kushinda mechi zao zilizobaki na kupata pointi zitakazowabakiza kwenye ligi uwezo huo wanao kama watafanya kwa pamoja, wachezaji, makocha na viongozi, msimu uliopita ulitunusuru kwa pointi tano na sasa wanaweza," alisema Yeya

Yeya aliwataka wachezaji kujitathimini upya wapi wamekosea na kuweka malengo ya ushindi ikiwemo mipango ya msimu ujao ili kuirudisha Mbeya City ya msimu wa kwanza.

Kwa sasa Mbeya City ambayo imekusanya pointi 24 pekee kwa kucheza mechi 24 inajiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wikiendi hii.

Post a Comment

 
Top