BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Kigali

HAKUNA ubishi tena, mpira ni mbinu, mengine mbwembwe tu. Hili limezidi kuthibishwa jana baada ya makocha wa Yanga Hans Van Pluijm na Juma Mwambusi kuamua kutumia mfumo wa kupanga mabeki watatu, viungo watano na washambuliaji wawili yani 3-5-2 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya APR.

Akizungumza na BOIPLUS baada ya mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Mwambusi alisema walijua APR wangetaka kushambulia sana ili kupata mabao mengi nyumbani kwao, hivyo wakaamua watumie mfumo ambao mpira ungechezwa zaidi katika eneo la kati.

"Tulifahamu kwavile wapo nyumbani basi lazima walikuwa wamejiandaa kushambulia zaidi na kupata mabao mengi, tukaona njia pekee ya kupunguza kasi yao ili isituletee madhara ni kuhakikisha tunacheza mpira pale katikati.

"Hivyo tukapanga mabeki watatu tu kwavile hawakuwa na kazi nzito sana, mipango mingi ya APR iliharibiwa na viungo wetu mahiri pale pale katikati wakati inaanzishwa." alisema Mwambusi akionekana ni mwenye kujiamini.Katika mchezo huo, APR walifanya mashambuli kadhaa lakini yalionekana kukosa madhara kwavile walipata upinzani mkubwa kutoka kwa Thaban Kamusoko, Vicent Bossou, Pato Ngonyani, Deus Kaseke na Haruna Niyonzima waliokuwa wakifuatana kama nyuki kwenye kupora mipira katikati ya uwanja.

Yawezekana katika mchezo wa marudiano makocha hao wakarejea mfumo wao wa siku zote wa 4-2-3-1 ambao utawaruhusu kushambulia sana huku viungo wawili pekee wakicheza chini kwa maana ya kukaba.

Post a Comment

 
Top