BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
KIUNGO Mshambuliaji wa Mbeya City, Ramadhan Chombo 'Redondo' amesema mchezo wao na Simba utakuwa mgumu kutokana na mazingira ya pande zote mbili.

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku timu zote zikihitaji ushindi baada ya kupoteza mechi zao zilizopita. Simba ilifungwa na Yanga wakati City walifungwa na Azam FC.

Chombo alisema kuwa kupoteza kwa mechi zao zilizopita ndiko kunaipa ugumu mechi hiyo hasa ukizingatia City inapigana kutoshuka daraja wakati Simba wao hawajakata tamaa na mbio za kuwania ubingwa wa VPL.

“Ni wazi mchezo utakuwa mgumu, hii ni kwa sababu kila timu inahitaji matokeo baada ya kupoteza mchezo uliopita, Simba ni timu nzuri na wako kwenye nafasi nzuri pia lakini wasitegemee kupata ushindi kwa sababu sisi tunauhitaji zaidi yao”,

“Tumeshinda mara kadhaa mbele ya Simba, hili ni jambo zuri kisaikolojia kwa sababu linaleta kujiamini, imani yangu kubwa dakika 90 za Jumapili zitakuwa upande wetu, ligi imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa na ina changamoto nyingi hasa kupanguliwa kwa ratiba mara kwa mara," alisema Chombo

Post a Comment

 
Top