BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar

Kipa wa Prisons, Beno Kakolanya ambaye amekuwa nguzo imara katika mafanikio ya timu hiyo

PRISONS inatarajia kucheza mechi ya Kombe la FA keshokutwa Alhamisi dhidi ya Azam FC, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam uwanja ambao Maafande hao wamekuwa na bahati nao.

Katika misimu miwili iliyopita Prisons imekuwa ikitoka sare na Azam ukiachana na msimu huu ambao walifungwa kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa bao 2-1.

Misimu miwili iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bao 2-2 na mechi ya msimu mwingine walitoka sare tasa hivyo matokeo ya Prisons kwenye Uwanja huo si mabaya kwao.

Kipa wa Prisons, Beno Kakolanya ameiambia BOIPLUS kuwa wamejiandaa vizuri na kujihakikishia ushindi utakaowapeleka hatua ya nusu fainali ambayo tayari Mwadui FC ya Shinyanga imetangulia kwa kuitoa Geita Gold Sports baada ya kuifunga mabao 3-0.

''Tumejiandaa vizuri na ni mechi ngumu ila tupo vizuri, Azam si wabaya lakini wana tatizo la kutokuwa makini katika safu ya ushambuliaji, mara nyingi wamekuwa wakifanya makosa ambayo ni faida kwetu.

''Huwa naheshimu safu zote za ushambuliaji kwa timu mbalimbali na mara kadhaa nawasisitiza hata mabeki wangu kuwa makini ili tusifungwe,''alisema Beno

Baada ya mechi hiyo Prisons itaelekea Mtwara ambako watacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC na baadaye kwenda Manungu kucheza na Mtibwa Sugar.

Post a Comment

 
Top