BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar


SERIKALI imetakiwa kuingilia kati suala la upangaji wa matokeo katika soka hususani ligi daraja la kwanza na kuzichukulia hatua za kinidhamu timu zote zinazohusika.

Akizungumza na BOIPLUS Mkurugenzi wa timu ya Friends Rangers Herry Mzozo alisema kanuni zinatungwa na watu wachache kwa kuzilinda baadhi ya timu na ndio maana matukio ya upangaji wa matokeo yanaongezeka kila Leo.

"Kanuni zinazotumika ni mbovu na ndani ya Bodi ya ligi kuna baadhi ya viongozi wanahusika katika sakata hilo kitu ambacho kinainyima haki klabu inayostahili, hivyo ni lazima.serikali iingilie kati jambo hili kwa lengo la kuunusuru mpira wa Tanzania." alisema Mzozo.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema masuala yote yanayohusu ligi yapo chini ya Bodi na lawama zote zielekezwe huko na si kwa Rais Jamali Malinzi japokuwa yeye ndio bosi wa soka.

"Bodi ya ligi kwa mujibu wa sheria ni chombo huru na hakiingiliwi na Mamlaka yoyote na mambo yanayohusu ligi yanaratibiwa hapo kwahiyo wao ndio wahusika katika matukio yote" alisema Mzozo.

Wikiendi iliyopita timu ya Stand FC ya Katavi ilishinda magoli 16-0 dhidi ya Kamazina FC kwenye mechi ambayo ni ya kumpata bingwa wa kuwakilisha mkoa huo mpya kwenye ligi daraja la kwanza.

Katika mechi za mwisho za ligi daraja la kwanza mwezi Februari kundi C timu ya Geita gold ya  mkoani Geita ilibuka na ushindi wa magoli 8-0 dhidi ya Kanembwa FC huku Polisi Tabora ikishinda magoli 7-0 dhidi ya JKT Oljoro michezo ambayo ilikuwa na harufu ya upangaji wa matokeo.

Post a Comment

 
Top