BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Tanga


UKIWAULIZA Yanga na Azam kuhusu Coastal Union wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani watakuambia potezea, lete stori nyingine. Lakini wekundu wa Msimbazi Simba leo wameitandika mabao 2-0 kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Coastal Union walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi ambapo katika dakika ya tano tu Ismail Mohamed alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuitumia vema krosi ya Juma Mahadhi. 

Baada ya hapo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku kosakosa zikitawala hadi dakika ya 39 ambapo Danny Lyanga aliipatia Simba bao la kwanza akimalizia krosi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Dakika ya 45 Tshabalala aliachia shuti kali ambalo lilipanguliwa na kipa Fikiri Bakari na mpira kuwakuta Lyanga na Hamis Kiiza ambao katika hali ya kushangaza walishindwa kuutumbukiza nyavuni.Kipindi cha pili Simba walionekana kutafuta bao la pili kwa nguvu huku wakiwatumia mabeki wao wa pembeni Tshabalala na Emery Nimubona kupandisha mashambulizi ambapo katika dakika ya 52, krosi maridadi ya Nimubona ilimkuta kinara wa mabao wa ligi kuu Kiiza na kuupachika nyavuni akiiandikia timu yake bao la pili.

Coastal hawakukata tamaa, waliendelea kutengeneza mashambulizi na katika dakika ya 66 Mahadhi alishindwa kufunga akiwa yeye na kipa Vicent Angban baada ya kazi nzuri ya Abdulhalim Humud kabla Hamis Ndemla naye hajapiga shuti kali lililotoka nje kidogo ya lango la Coastal.

Kocha wa Simba Jackson Mayanja aliwapumzisha Ndemla na Mwinyi Kazimoto na kuwaingiza Awadh Juma na Mussa Mgosi na kwa upande wa Coastal alitoka Ibrahim Twaha, Ismail Mohamed na Ally Shiboli na huku nafasi zao zikichukuliwa na Chidiebele Abasilim, Ayoub Yahaya na Said Jailan.

Kufuatia ushindi huo Simba imeendelea kuongoza ligi sasa ikiwa imefikisha pointi 57 kwa mechi 24 ilizocheza huku ifuatiwa na Yanga na Azam zenye pointi 50 kila moja zikiwa zimecheza mechi 21. Kwa upande wa wafungaji Kiiza anaongoza kwa mabao 19 akifuatiwa na Tambwe mwenye 17.

Huko mjini Songea, Majimaji imefumua Mbeya City mabao 3-1. Mabao ya Wanalizombe yakifungwa na Danny Mrwanda (2) na Marcel Kaheza huku lile la City likifungwa na Abdallah Juma.

Post a Comment

 
Top