BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar


WEKUNDU wa Msimbazi Simba leo imeifunga Mbeya City mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kipindi cha kwanza kilimalizika bila bao lolote kutinga nyavuni licha ya kosakosa kadhaa. Kwa upande wa Simba, kushindwa kujipanga kwa washambuliaji wake Hamis Kiiza na Ibrahim Ajibu kuliwanyima nafasi nyingi za kufunga kwavile kila mara walionekana kuotea.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Jackson Mayanja ya kumtoa Brian Majwega na kumuingiza Danny Lyanga huku Emery Nimuboma na Hamis Kiiza wakiwapisha Ramadhan Kessy na Awadh Juma yalionyesha kuzaa matunda kwani timu hiyo ilianza kufanya mashambulizi makali yaliyopelekea kupata bao katika dakika 75 likifungwa na Lyanga.


Baada ya bao hilo Simba walionekana kuridhika na kupunguza mashambulizi jambo lililopelekea City wahamishie makazi yao langoni mwao. Kama si kukosa umakini kwa washambuliaji wa City basi matokeo yangeweza kubadilika.

Katika dakika ya 90, Ajibu aliambaa na mpira na kuwalamba chenga mabeki wa City kisha kufunga bao safi lililowahakikishia Simba nafasi ya kukaa kileleni mwa ligi kwa kufikisha pointi 48 ikifuatiwa na Yanga na Azam zenye pointi 47 kila moja.


Post a Comment

 
Top