BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kimemaliza salama mazoezi yake ya mwisho asubuhi hii katika  uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku makocha na wachezaji wakijinasibu kuwafurahisha watanzania hapo kesho.

Wachezaji wote wa Stars inayojiandaa na mchezo dhidi ya Chad wapo fit isipokuwa Mwinyi Kazimoto pekee ambaye hata leo ameshindwa kufanya mazoezi na wenzake akiugulia maumivu ya nyonga aliyoyapata katika mchezo wa awali uliopigwa nchini Chad.

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta ameiambia BOIPLUS kuwa wana kila sababu ya kupata ushindi kesho kwavile licha ya kwamba morali ya wachezaji iko juu, lakini pia maelekezo waliyoyapata toka kwa walimu wao yamewaongezea vitu zaidi.

"Kama ulivyoona wachezaji wote wana furaha na wanaonyesha kujiamini, hii inaleta matumaini kuwa ari ya ushindi ipo. Lakini pia walimu wameona mapungufu yaliyotokea Chad, wameyafanyia kazi, tuombe Mungu tuamke salama tutapata ushindi bila shaka." alisema Samatta anayeichezea KRC Genk ya Ubelgiji

Kwa upande wa kocha msaidizi Hemed Morocco alisema wanahitaji ushindi katika dimba la nyumbani, wamejipanga kuonyesha 'njaa' toka dakika ya kwanza ya mchezo hadi mwisho.

"Timu iko vizuri hivyo lengo letu la kupata ushindi litafanikiwa bila shaka, tutaanza kutafuta mabao  tangu dakika za mwanzoni. Watanzania wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono." alisema Morocco

Pambano la Stars na Chad litapigwa kuanzia majira ya saa 10 alasiri kwenye uwanja wa taifa  na kiingilio cha chini kitakuwa ni sh 5,000.

Post a Comment

 
Top