BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
KLABU ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza kwa kushirikiana na kampuni ya uchimbaji wa madini ya ACACIA imeingia makubaliano ya kuendeleza soka la vijana nchini.

Makamu wa Rais wa kampuni ya ACACIA Deo Manyika amesema kuwa wameingia ubia na klabu hiyo kwa ajili ya kuendeleza soka la vijana na kwa kuanzia watawatafuta nchi nzima ikiwa ni pamoja na kuandaa makocha vijana ambao watakuwa msaada kwa taifa katika siku zijazo.

"Tutatafuta vijana nchi nzima ili kuendeleza vipaji vyao, hii itakwenda sambamba na uandaaji wa makocha vijana. Nchi zote zilizoendelea duniani kote lazima ziliwekeza katika soka la vijana, " alisema Manyika.

Kwa upande wake Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF Jamal Malinzi amesema ubia huo umekuja kipindi muafaka huku Tanzania ikiwa mwenyeji wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika mwaka 2019 na kutanabaisha kuwa itawasaidia kuandaa timu nzuri itakayoleta mafanikio katika ardhi ya nyumbani.

"Sisi kama TFF tutahakikisha tunatoa ushirikiano wa asilimia mia moja katika ubia huu kwa kuwa sisi ndio tunanufaika zaidi ukizingatia tutakuwa wenyeji ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019." akisema Malinzi

Malinzi pia ameitaka klabu ya Stand United inayodhaminiwa na kampuni ya ACACIA kuacha migogoro hususani katika masuala ya fedha kitu ambacho kinaweza kuwakimbiza wadhamini hao.

"Hakuna mtu ambaye anaweza kuwekeza fedha zake mahali ambapo hana uhakika na matumizi yake kwahiyo hii migogoro ndani ya Stand inaweza kuwakimbiza wadhamini na sisi hatuko tayari kuona tunashindwa kufanikiwa kutokana na hilo" alisema Malinzi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa masoko wa klabu ya Sunderland, Gary Hutchson alisema ubia huu utakuwa msaada kwa nchi na kama utafanikiwa basi wataangalia uwezekano wa kudhamini michezo mingine.

Post a Comment

 
Top