BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar

BAADA ya timu ya taifa ya Chad kujitoa kwenye kundi G la michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) 2017, kundi hilo limebaki na timu tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Tanzania.

Tayari timu hizo zote zilishapata ushindi wa awali kwa Chad hivyo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa michuano hiyo timu hizo zimepokwa pointi tatu kila moja hivyo msimamo wa kundi kubadilika huku Misri ikiongoza ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Nigeria yenye mbili na Tanzania yenye pointi moja.

Soka lina miujiza yake, na kama miujiza hiyo ikitokea kwa 'kuibeba' Taifa Stars basi watanzania wanaweza wasiamini macho yao watakapoiona nchi yao ikifuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika nchini Gabon mwakani.

Hebu tazama hapa, kila timu imebakiwa na michezo miwili. Endapo ikatokea Nigeria ikaenda kulazimisha sare nchini Misri, maana yake ni kwamba Misri itakuwa na pointi tano huku Nigeria wakifikisha tatu. Baada ya hapo Misri atalazimika kuifuata Stars, ikitokea akapoteza maana yake ni kwamba atakuwa amemaliza michezo akiwa na pointi tano pekee huku Stars ikifikisha nne. Kwahyo fainali ya nani ataenda AFCON itafanyika nchini Nigeria.

Stars itaifuata Nigeria ikiwa inajua kuwa endapo itashinda basi itafuzu moja kwa moja kwa fainali za AFCON. Lakini nimetumia neno 'Miujiza'. Ni kweli miujiza, tena miujiza miwili ndio inahitajika ili Stars ifuzu. Kwanza Nigeria ipate sare nchini Misri, pili Stars ikapate ushindi nchini Nigeria.

Soka lina mambo yake ya ajabu, ishawahi kuwastaajabisha watu wengi sana, lakini bado huu ni mchezo wa wazi. Hivyo ni vema watanzania wakasubiri miujiza lakini pia wasisahau kuwa soka huchezwa hadharani.

Post a Comment

 
Top