BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), jana ilikamata magari matano ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kile kilichoelezwa ni deni la kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kubaini kwamba TFF inadaiwa Sh 1.118 bilioni.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo amethibitisha kukamata kwa magari hayo ambayo yamehifadhiwa kwenye eneo la kuuzia magari linalomilikiwa na Yono Action Mart ambao wanafanya kazi ya kukamata mali kwa kushirikiana na TRA.

Kayombo alisema kuwa madeni hayo ni pamoja na yale ambayo hayajamalizwa kulipwa baada ya kufungia akaunti zao za benki kwa kushindwa kulipa kodi za makocha wao wa kigeni na sasa madeni yaliyobainiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT), makato ya wafanyakazi wote wa TFF pamoja na wachezaji wa kigeni, kodi ya 'skill and development levy' (SDL).

"Tumewapa taarifa kwa maandishi juu ya kufuata masharti ya kukomboa magari yao, endapo watashindwa kulipa basi yatauzwa, yote hayo yamebainika baada ya kufanya ukaguzi," alisema Kayombo

Maafisa wa TFF walipotafutwa kutoa maelezo kuhusiana na tukio hilo walikuwa hawapokei simu na wakati mwingine ilijibiwa kuwa inatumika.

Post a Comment

 
Top