BOIPLUS SPORTS BLOGWASANII  mbalimbali wa muziki hapa nchini jumamosi wanatarajiwa kukinukisha katika Viwanja vya Mwembe Yanga Temeke jijini Dar es Salaam katika tamasha la Amsha Mama Festival.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake, Balozi wa tamasha hilo  Khalid Ramadhani ‘Tundaman’, ambaye amepewa Ubalozi  huo kupitia waandaaji wa tamasha la (AFWAB)  AMSHA MAMA Festival 2016, lililo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa lebo ya Candy na Candy   Records Joe Kariuki, alisema tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Machi 5 mwaka huu katika uwanja wa Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.

Tundaman alisema maandalizi ya shoo hiyo tayari yameshakamilika kwa kiasi kikubwa hivyo angependa kutumia fursa hii kuwaalika wakazi wote wa jiji la Dar, kujumuika siku hiyo kushuhudia burudani mbalimbali zitakazotolewa na wasanii kibao ambao tayari wemethibitisha kufanya makamuzi siku hiyo.

 “Tunapenda kuwaalika Watanzania wote kwa ujumla siku ya jumamosi waje kwa wingi katika Viwanja vya Mwembe Yanga ili tujumuike kwa pamoja katika tamasha la kuhamasisha wanawake kujikwamua katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi." alisema Tundaman

Tundaman aliongeza kuwa tamasha hilo litakuwa ni la wazi kwa maana kwamba watu wote watapata burudani nyingi bila malipo yoyote hivyo waje kuwashuhudia wasanii kama, Khadija Kopa, Mr Blue, Snura, Msaga Sumu, Ali Chocky na Tunda Man  mwenyewe wakitoa burudani ya hali ya juu huku akisisitiza ulinzi na usalama siku hiyo ni wa uhakika.

Kwa upande wake Kariuki, ambaye ni mratibu mkuu wa tamasha hilo amewaomba akina mama wanaojishughulisha na biashara mbalimbali hususani mama ntilie, wauza matunda na wauzaji wa mitumba wajitokeze kwa wingi kuja kunadi bidhaa zao  siku hiyo kwani hiyo ndiyo fursa yao ya kipekee ya kujitangaza bure.

Post a Comment

 
Top