BOIPLUS SPORTS BLOG


KIKOSI cha timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu 'Twiga Stars', leo kimefanya mazoezi ya mwisho tayari kwa kuwakabili timu ya Taifa ya Wanawake kutoka Zimbabwe 'Mighty Warriors' katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kesho Ijumaa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.

Twiga Stars inayonolewa na kocha mzawa mwanamke, Nasra Juma imekamilisha ratiba yake leo asubuhi kwa kufanya mazoezi mepesi katika uwanja wa Karume zilipo ofisi za TFF, huku kocha huyo akisema vijana wake wote wapo katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo huo.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa TFF uliopo Karume, Nasra amesema ana waheshimu Zimbabwe wana timu nzuri, ndani ya miaka minne wameshacheza nao zaidi ya mara nne, mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita wameyafanyi kazi na hivyo kesho ana imani watafanya vizuri.

Aidha kocha Nasra, amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kesho Ijumaa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi kuwapa 'support' Twiga Stars katika mchezo huo utakaonza majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Naye nahodha wa kikosi hicho Sophia Mwasikili, amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri, wana ana ari na morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo wa kesho, na kuwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuja kuwashangilia uwanjani watakapokuwa wakipeperusha bendera ya Tanzania.

Wapinzani wa Twiga Stars, timu ya taifa ya Zimbabwe wanawasili leo jioni tayari kwa mchezo huo, huku waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Ethiopia wakiwa tayari wameshawasili leo mchana kwa ndege ya  shirika la ndege la Kenya (KQ).

Post a Comment

 
Top