BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Chamazi
TIMU ya Taifa ya Wanawake 'Twiga Stars' imekubali kipigo cha bao 2-1 dhidi ya Zimbabwe katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Afrika kwa wanawake, mechi ambayo imepigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Twiga ndiyo ilikuwa ya kwanza kuona nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 17 kupitia kwa mchezaji wao Mwanahamis Omary baada ya kupigiwa mpira mrefu na Asha Rashid 'Mwalala'.

Wakati mashabiki wa Twiga wakiwa bado wamesimama wakishangilia bao hilo, walijikuta furaha hiyo inapotea ghafla baada ya Zimbabwe kusawazisha bao hilo dakika ya 19 kupitia kwa mchezaji wao Erina Jeke.

Mwamuzi wa mchezo huo Tsige Sisay kutoka Ethiopia alimpa kadi ya njano Eunice Chibanda baada ya kumchezea rafu Stumai Abdallah wa Twiga Stars huku kadi nyingine ya njano ikienda kwa Emmaculate Msipa aliyemfanyia madhambi Fatuma Issa.

Dakika ya 46 Zimbabwe iliongeza bao la pili mfungaji akiwa ni yule yule aliyepachika bao la kwanza Erina aliyepiga shuti akiunganisha mpira wa  krosi iliyopigwa na Majory Nyauwe.

Twiga Stars italazimika kusafiri kwenda Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ambapo itahitaji ushindi mnono wa ugenini ili iweze kusonga mbele.

Post a Comment

 
Top