BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda

MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Thomas Ulimwengu jana amecheza mchezo wake wa kwanza tangu apate maumivu ya misuli ya paja mwezi januari, na kuchangia upatikanaji wa mabao yote mawili katika sare ya mabao 2-2 waliyoipata dhidi ya St George ya nchini Ethiopia.

Wenyeji walianza kupata bao katika dakika ya 11 kupitia kwa Assefa Behailu katika uwanja wa Bahir Dar kabla Ulimwengu hajamtengenezea bao zuri la kusawazisha Daniel Adjei katika dakika ya 45 ya mchezo huo.


Mara baada ya kuanza kipindi cha pili, Ulimwengu alifumua shuti kali ambalo lilimgonga beki wa St George, Isaac Isiende na kutinga nyavuni lakini Girma Adane aliisawazishia timu hiyo kwenye dakika ya 60.


Ulimwengu ambaye alitoka dakika ya 63 na nafasi yake kuchukuliwa na Roger Asale aliiambia BOIPLUS kuwa amefurahi kuisaidia timu yake ingawa bado hajawa fit kabisa.


"Nashukuru nimechangia upatikanaji wa sare hii ya ugenini, hata hivyo bado sijawa fit moja kwa moja kwavile si unajua tena mtu ukitoka majeruhi maumivu hayawezi kupotea kabisa mara moja. " alisema Ulimwengu.


Kwa sare hiyo waliyoipata, Mazembe  katika mchezo wa marudiano jijini Lubumbashi watahitaji ushindi wowote, sare ya bao 1-1 au suluhu ili kusonga hatua ya pili ya ligi hiyo ya mabingwa Afrika.

Post a Comment

 
Top