BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Tanga


WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) wamepiga marekebisho ya Katiba hasa kipengele cha kupunguza idadi ya wapiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa hoteli ya Naivera, jijini Tanga. 

TFF tayari iliandaa Katiba ambayo ilikuwa na mabadiliko hayo yanayosemekana kuwa ni maelekezo ya FIFA jambo ambalo wajumbe hao wamelipinga vikali na kwamba liwekwe pembeni mpaka mkutano mkuu ujao hivyo ajenda nyingine 11 zilizojadiliwa zilipitishwa, ajenda ya kipengele hicho ilikuwa ya 11 kati ya ajenda 12.

Mabadiliko hayo yalikuwa yakielekeza kwamba wapiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa TFF wanapaswa kuwa Wenyeviti pekee huku Makatibu na vyama vingine ambavyo vinashiriki vikipigwa chini hivyo endapo wangepitisha ilikuwa ni idadi ya wajumbe 28 pekee kutoka Tanzania nzima ambao wangepaswa kupiga kura.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mabadiliko ya Katiba yameelekeza pia kuwa vyama vya mikoa viwe na Makatibu wa kuajiriwa na si kuchaguliwa huku nafasi ya kiongozi wa kuchaguliwa ibaki kuwa ya Mwenyekiti pekee.

"Ni wazo zuri kuwa na Katibu wa kuajiriwa, lakini je tumejipanga vipi kuwalipa mishahara wakati hao tu walioajiriwa na Klabu ambazo angalau zina udhamini wanashindwa kuwalipa makatibu wao? Halafu kupunguza idadi ya wapiga kura ni kuhalalisha mfumo wa utoaji rushwa kwenye uchaguzi kwani idadi ndogo ya wapiga kura kila mgombea anaweza kuimudu kuinunua.

"Hivyo kwa pamoja tumekubaliana kwamba hiyo ajenda isijadiliwe, tupewe muda wa kutafakari kwa kina mpaka Mkutano Mkuu ujao, wengi hawajasoma, tumeikuta humu humu ndani baada ya kuingia sasa tutajadili nini," alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo

Akizungumza mara baada ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema "Tangu mkutano mkuu uliopita ambao tulifanyia Morogoro tuliwapa taarifa hizi za mabadiliko ya Katiba na walikubali tujadili kwenye mkutano huu, ila sasa wanadai hawana taarifa wakati tuliwatumia Wenyeviti wote wa mikoa.

"Hapa tunafuata demokrasia ambapo sisi tutawafanya mawasiliano na Fifa ambao wametoa maelekezo hayo kwani itafikia muda ni lazima mabadiliko yafanyike pasipo kuyakwepa, ila sasa tunawasikiliza wajumbe maoni yao," alisema Mwesigwa.

Mkutano huo uliongozwa na Rais wa TFF Jamal Malinzi na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza.

Post a Comment

 
Top