BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Waandishi Wetu
YANGA na Azam zimetinga hatua ya nusu fainali za michuano ya Kombe la FA baada ya kushinda mechi zao za leo za robo fainali hivyo wametangulia kuisubiri Simba itakayocheza April 7 dhidi ya Coastal Union.

Yanga imeifunga Ndanda bao 2-1 huku Azam wakishinda bao 3-1 dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya hivyo Yanga na Azam wanaungana pamoja na Mwadui walioitoa Geita Gold Sports kwa bao 3-0.


Yanga ilianza kwa kasi mechi hiyo ambapo dakika ya nne straika wake Paul Nonga alikosa bao baada ya kupiga shuti ambalo lilipanguliwa na kipa wa Ndanda Jeremiah Kisubi ikiwa ni pasi ya winga wao Simon Msuva.


Dakika sita baadaye straika wa Ndanda Atupele Green alijibu shambulizi hilo kwa kuifungia bao timu yake lakini mwamuzi wa mchezo huo alilikataa bao hilo kwa madai kuwa aliotoea na kusababisha mwamuzi wa mechi hiyo Jimmy  Fanuel kutoka Shinyanga kutoa kadi ya njano kwa Salvatory Ntebe ambaye alitoa lugha kali akilalamikia kunyimwa bao halali.


Hata hivyo Nonga aliweza kuifungia timu yake bao la kwanza kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliyopigwa na Juma Abdul dakika ya 27 baada ya Kigi Makassy kumchezea rafu Donald Ngoma bao ambalo lilidumu mpaka mapumziko.


Mchezaji wa Ndanda, Omary Mponda alipoteza nafasi ya wazi dakika ya 25 akiwa ndani ya eneo la hatari kwani shuti lake liliokolewa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ikiwa ni pasi ya Atupele huku Msuva akishindwa kuipatia bao timu yake baada ya shuti lake kugonga mwamba na kutoka nje ikiwa ni pasi ya Thaban Kamusoko.

Kipindi cha kwanza, Yanga ilipata nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia kutokana na washambuliaji wao kukosa umakini.

Dakika ya 56, Ndanda walifanikiwa kusawazisha bao la kwanza kupitia kwa mchezaji wao Makassy aliyepokea pasi ya Braison Raphael iliyotokana na shambulizi la kushitukiza kabla ya Kevin Yondani kuifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya Msuva kuangushwa .


Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm aliamua kufanya mabadiliko ambapo aliwatoa  Pato Ngonyani, Deus Kaseke na Kevin Yondani nafasi zao zilichukuliwa na Salum Telela na Geofrey Mwashiuya pamoja na Nadir Haroub wakati kocha wa Ndanda Abdul Mingange alimtoa Salvatory Ntebe na kumwingiza Ahmed Msumi alitoa Mponda aliingia Salim Minely.Kwa upande wa Azam, timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1, bao la Azam lilifungwa dakika ya kumi na Shomary Kapombe akiunganisha pasi ya Didier Kavumbagu wakati Jeremiah Juma akiisawazishia timu yake dakika ya 32 baada ya beki Aggrey Morris kuteleza na hivyo straika huyo kuuwahi mpira huo na kuutia nyavuni kabla ya Kapombe hajaongeza bao la pili dakika ya 50 kwa shuti kali.


Khamis Mcha alifunga ukurasa wa mabao kwa kuifungia Azam bao la tatu dakika ya 80 na kuifanya timu hiyo itoke na ushindi mnono.


Baada ya mchezo huo kocha wa Azam, Stewart Hall aliwaambia waandishi wa habari luwa amefurahishwa na matokeo hayo kwavile hakuyatarajia kutokana na kikosi chake kutokuwa fit akiwataja Kapombe na John Bocco wamecheza wakiwa wana mafua makali.

Post a Comment

 
Top