BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar

TIMU za Yanga na Azam zimeshinda jana katika michezo yao ya michuano ya CAF, lakini hapa Tanzania ligi kuu inaendelea na Mnyama Simba ameendelea kutisha leo baada ya kuifunga Prisons bao 1-0  kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kipindi cha kwanza timu hizo zilicheza kwa umakini mkubwa huku Simba wakitumia mtindo wao wa siku zote wa pasi fupi fupi wakati Prisons wao wakijaribu 'kuwakataa' Simba kwa kupiga pasi ndefu.

Nusura Ibrahim Ajibu aipatie Simba bao katika dakika ya 33 baada ya kupitishiwa krosi maridadi na Hamis Kiiza.

Dakika ya 49, straika 'kiwembe' wa Prisons, Jeremia Juma alipiga kichwa mpira ambao kipa wa Simba Vicent Angban alishindwa kuuokoa lakini ukagonga mwamba.

Golikipa anayeng'ara zaidi kwasasa hapa nchini, Benno Kakolanya aliuthibitishia umma kuwa sasa ameiva haswa baada ya kuokoa shuti kali la Ajibu ambapo watu wengi waliokuwa wanatazama mchezo huo waliamini hilo lingekuwa bao kwa Simba.Dakika zilivyozidi kuyoyoma Simba waliongeza umakini katika mipango yao ya kutafuta bao ndipo kiungo asiyesifika sana lakini mwenye msaada mkubwa ndani ya Simba, Awadh Juma 'Maniche' alipoipatia timu yake pointi tatu muhimu baada ya kufunga bao zuri akifumua shuti kali la nje ya 18.

Kocha wa Simba Jackson Mayanja aliwapumzisha Mussa Hassan 'Mgosi', Kiiza na Justice Majabvi nafasi zao zikichukuliwa na Danny Lyanga, Raphael Kiongera na Awadh. Prisons wao waliwatoa Jeremia Juma na Juma Seif na kuwaingiza Meshack Seleman na Freddy Chudu.

Kwa matokeo hayo Simba inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 54 ingawa inaizidi Yanga kwa michezo miwili na Azam michezo mitatue. Yanga ina pointi 50 na Azam ina 47

Post a Comment

 
Top