BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda na Zainabu Rajabu, Dar


TIMU ya Yanga leo imefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika kwa kuitoa APR ya Rwanda baada ya leo kutoka sare ya bao 1-1. Mechi hiyo imechezwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

APR  ambao walipoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-1 jijini Kigali, waliwashtua Yanga mapema katika dakika ya tatu tu pale winga Fiston Nkinzingabo  alipoifungia timu yake bao zuri akimalizia krosi ya Rusheshangonga Michel.

Baada ya bao hilo APR walionekana kutawala mchezo lakini Yanga waliendelea kutulia na kufanya mashambulizi kadhaa huku Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko wakipoteza nafasi za kufunga. 

Dakika ya 28 pasi ya Tambwe ilimkuta Donald Ngoma akiwa katikati ya mabeki wa APR lakini alifanikiwa kugeuka na kuwatoka kabla hajaachia shuti kali lililojaa wavuni na kumuacha kipa Jean Claude Ndoli akichupa bila mafanikio.

Kipindi cha pili timu hizo zilicheza mpira wa wazi kila mmoja akifunguka ili kupata bao na kushambuliana kwa zamu ingawa kukosa umakini kwa washambuliaji wa timu hizo kulisababisha kusiwe na bao la ziada.

Katika mchezo huo kocha wa Yanga Hans Van Pluijm aliwapumzisha Haruna Niyonzima na Deus Kaseke huku akiwaingiza Simon Msuva na Geofrey Mwashiuya. Kwa upande wa APR, Nizar Kanfir aliwatoa Nkinzingabo na Benadata Janvier nafasi zao zikichukuliwa na Djihad Bizimana pamoja na Betrand Iradikunda

Kwa matokeo hayo Yanga imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 hivyo kusubiri hadi usiku itakapojua itapambana na nani kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Al Ahly ya Misri.

Post a Comment

 
Top