BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Kigali
TIMU ya Yanga leo imthibisha kuwa wao ni wa kimataifa baada ya kuitandika APR mabao 2-1 katika mchezo wa Klabu bingwa Afrika uliochezwa kwenye dimba la Amahoro.

Kipindi cha kwanza APR ilifika langoni mwa Yanga mara nyingi lakini walionekana wazi kuzidiwa mbinu na walinzi wa ngome ya Yanga iliyoongozwa na Vicent Bossou na Kelvin Yondan. 

Dakika ya 20, Juma Abdul aliwainua mashabiki wa Yanga kwa bao safi kufuatia shuti kali la mpira wa adhabu ndogo uliotinga moja kwa moja nyavuni huku kipa wa APR, Kwizera Oliver akichupa bila mafanikio.


Kipindi cha pili APR waliliandama lango la Yanga lakini umakini wa mabeki wa wanajangwani hao pamoja na kipa Ally Mustapha uliwanyima bao wanajeshi hao.

APR walioonyesha kuchanganyikiwa kadiri dakika zinavyokwenda, almanusura wapate bao katika dakika ya 55 baada ya beki mahiri Rwatubyaye Abdul kuachia shuti kali ambalo lilimgonga Pato Ngonyani kabla mpira huo haujaokolewa na mabeki wa Yanga. Wachezaji wa APR walimzonga mwamuzi wakidai Pato aliunawa mpira huo.

Heka heka langoni mwa Yanga ziliendelea huku Yanga wakiongeza umakini na kucheza kwa tahadhari wakiumudu vema mfumo wao wa 3-5-2. 

Mashambulizi ya kushtukiza yalionekana kuiletea faida Yanga kwani katika dakika ya 74, Thaban Kamusoko aliipatia Yanga bao la pili akimalizia pasi nzuri ya Donald Ngoma.

Katika dakika za nyongeza, Patrick Sibomana aliiandikia APR bao la kufutia machozi hivyo mchezo huo kumalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kwa ushindi huo Yanga wamejitengenezea mazingira mazuri ya kuitoa APR kwani katika mchezo wa marudiano jijini Dar watahitaji japo sare tu kuiondosha timu hiyo mashindanoni.

Post a Comment

 
Top