BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma na Zainabu Rajabu

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika timu ya Yanga inashuka dimbani kesho Jumamosi katika uwanjani wa Taifa kuwakabili mabingwa wa kihistoria wa kombe hilo Al-Ahly toka Misri.

Mwaka huu ni wa 24 kwa Yanga  kushiriki ligi ya mabingwa Afrika lakini haijawahi kufika mbali zaidi ya kutolewa katika raundi ya awali au ikizidi sana raundi ya pili na hasa inapokutana na timu kutoka Kaskazini na Magharibi mwa Afrika.

Mwaka huu Yanga wameonekana kupania kufika mbali wakianzia kwenye usajili hadi maandalizi ya timu kuelekea michezo hiyo. Kuelekea mchezo wa kesho, kauli kadhaa zimetolewa, BOIPLUS imepita hapa na pale kusikia chochote kinachoonhelewa.

Mwambusi na matumaini kibao
Kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mwambusi amesema anakiamini kikosi chake ambacho kinacheza vizuri na wachezaji wanajua wanachotakiwa kufanya huku akijinasibu kuwa wamewapa mafunzo maalum kwa ajili ya kutumia nafasi zinazopatikana.


"Tunaiheshimu Al Ahly ni timu kubwa na ina historia kubwa barani Afrika ila hatuwahofii, tutakacho fanya ni kuwadhibiti ili tuwafunge hasa katika ardhi ya nyumbani," alisema Mwambusi.

Tambwe ataka wenzake 'wakomae'
 Mshambuliaji tegemeo wa klabu hiyo Amissi Tambwe amesema wanatakiwa tupigane kufa na kupona kuwatoa ili wafute uteja kwao jambo ambalo anaamini linawezekana kabisa.

 "Wachezaji wote tunapaswa tujitume hadi tone la mwisho na inawezekana kuwatoa hasa kama tutapata matokeo mazuri nyumbani".

Juma Abdul amhofia Mgabon
 Beki wa kulia ambaye yupo katika ubora mkubwa Juma Abdul amesema wamewahi kucheza na mabingwa hao zaidi ya mara tatu lakini hawakuweza kuwatoa na sasa ni zamu ya mafarao kutoka kwavile watoto wa Jangwani wamedhamilia kufanya hivyo licha ya ubora walionao hasa mshambuliaji wao Malick Evouna.


" Tumejidhatiti kuwatoa Al Ahly ila kuna mshambuliaji wao raia ya Gabon anaitwa Malick ni hatari sana tunapaswa kumchunga na hatupaswi kumpa nafasi ya kutuadhibu."

Jeuri ya Yanga iko hapa
Yanga inawategemea washambuliaji Donald Ngoma na Tambwe ambao waneonesha ushirikiano mzuri na kusaidia upatikanaji wa zaidi ya robo tatu ya ushindi kwa timu hiyo huku katika idara ya kiungo wakimtegemea fundi wa mpira Thaban Kamusoko na Pato Ngonyani au Salum Telela kwa ajili ya kuunganisha timu hiyo.

Kwa miaka yote Yanga wamekuwa wakali kwenye kushambulia kupitia pembeni, mawinga wanaoitia kiburi timu hiyo ni Simon Msuva na Deus Kaseke kwa ajili ya kuwakimbiza waarabu. Kwa upande wa idara ya ulinzi Kelvin Yondani na Vincent Bossou watasimama katikati huku Haji Mwinyi na Abdul wakicheza kama mabeki wa pembeni ambao licha ya kusaidia kumlinda kipa (Deo Munish au Ally Mustafa), pia watakuwa na kazi ya kupandisha mashambulizi.

Canavaro hati hati kuwavaa waarabu
Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub Canavaro anaweza asicheze mchezo huo kutokana na ukubwa wa mechi huku yeye tangu atoke kwenye majeruhi akiwa amecheza dakika 90 mechi moja tu ya kombe la FA dhidi ya Singida United kitu ambacho kinaweza kumfanya kocha Hans aamue  kumuweka benchi.

Historia inaibana Yanga
Kabla ya fainali za mwaka huu mara ya mwisho timu hiyo kushiriki ligi ya mabingwa Afrika ilikuwa ni mwaka juzi ambapo timu hiyo ilitolewa na Al Ahly kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1. Yanga walishinda bao 1-0 nyumbani na katika mchezo wa marudiano Ahl nao wakashinda 1-0 na kuamuriwa zipigwe penati.


Baada ya hapo msimu uliofuata Yanga ilikosa ubingwa ikamaliza msimu nafasi ya pili ambapo ilishiriki kombe la Shirikisho huku ikionekana kujipanga kiasi kwa kufika hadi raundi ya tatu kabla ya kutolewa na Etoile du Sahel kwa mabao 2-1.

Yanga ilianza vizuri kwa kuwatoa Cercle de Joachim ya Mauritius na baadae APR ya Rwanda kabla ya kukutana na Al Ahly mechi itakayochezwa kesho kabla ile ya marudio itakayopigwa Aprili 19 jijini Cairo.

Mwaka 2012 Yanga ilikuwa bingwa wa Tanzania na kushiriki michuano ya Ligi ya mabingwa safari hiyo iliaga mapema michuano hiyo kwani mchezo wa raundi ya kwanza ilipangiwa Zamalek ya Misri na haikuweza kufua dafu baada ya kutupwa nje kwa jumla ya mabao 2-1.

Yanga waitafuta rekodi ya Mnyama
 Mwaka 2003, Simba iliweka rekodi ya kuwavua ubingwa wa Afrika Zamalek, hiyo ilikuwa ni baada ya  Simba kupata ushindi wa bao 1-0 uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na Zamalek kupata ushindi kama huo katika mechi ya marudiano iliyopigwa Cairo Misri. Baada ya hapo Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi kwa mikwaju ya penati ingawa haikufurukuta tena.

Yanga wamejiandaa kuiondosha Al Ahly katika ardhi yao ya nyumbani ili kuvunja rekodi ya Simba. Ni wazi kuwa ili wafanikiwe katika hilo wanapaswa kupata matokeo chanya katika dimba la Taifa hapo kesho.

BOIPLUS inawatakia Yanga kila la heri katika mchezo huo

Post a Comment

 
Top