BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar

ILE kiu ya muda mrefu ya wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba kuona timu yao inamiliki Uwanja wao wenyewe inaelekea kukatwa baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwa kwenye hatua za mwisho kuanza ujenzi.

Akizungumza na BOIPLUS, Rais wa klabu hiyo Evans Aveva alisema kuwa Kamati ya Ujenzi wa uwanja huo inasubiri kukabidhiwa michoro na gharama za ujenzi wa uwanja ili iendelee na hatua inayofuata.

"Mkandarasi anakamilisha kazi yake ya awali ili kutujuza gharama za jumla za ujenzi wa uwanja wetu, nadhani hadi Jumanne hivi tunaweza kuwa tumejua.

"Tukipewa mahesabu hayo sisi tutayakabidhi kwa ile kamati ili wao sasa waitishe mkutano wa waandishi wa habari na kuwaeleza mipango yao," alisema Aveva.

Kamati ya ujenzi wa uwanja huo inaundwa na Mwenyekiti Zacharia Hans Poppe, Makamu Mwenyekiti Salim Muhene, Katibu Issa Batenga na wajumbe watano ambao ni Cressentius Magori, Imani Kajula, Ally Suru, Adam Mgoi na Gerry Ambi.

Kwa mujibu wa Aveva, ujenzi huo utahusisha uwanja wa mpira wa nyasi asilia ambao utatumika kwa ajili ya mechi, uwanja wa mazoezi ambao utakuwa na nyasi bandia, hosteli kwa ajili ya wachezaji, Ofisi kwa ajili ya viongozi wa Simba na 'Gym'.

Post a Comment

 
Top