BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Chamazi
TIMU ya Azam FC imerejea kwenye mbio za kuutafuta ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara baada ya kuwafunga Majimaji ya Songea  magoli 2-0 katika uwanja wa Chamazi Complex

Majimaji waliuanza mpira kwa kasi na kufanya mashambulizi makali langoni mwa Azam ambapo dakika ya saba kiungo Peter Mapunda alikosa goli la wazi baada ya shuti lake kutoka pembeni ya goli.

Dakika ya 15 mshambuliaji Danny Mrwanda alipata nafasi ya kuifungia timu yake goli lakini golikipa Aishi Manula alikuwa makini langoni na kuondosha hatari hiyo.

Azam nao walianza kulisakama lango la Majimaji na dakika ya 33 Hamis Mcha Vialli alipiga shuti kali lakini golikipa David Burhani alipangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mpaka wanaenda mapumziko hakuna timu iliyokuwa nimepata goli.

Kipindi cha pili Azam walifanya mabadiliko ya kumtoa Didier Kavumbagu na kumuingiza Ame Ally Zungu na kuongeza kasi kwa wana lambalamba ambapo dakika ya 50 Mudathir Yahaya aliwapatia wenyeji goli la kuongoza baada ya kupokea krosi safi ya Ramadhani Singano.

Dakika ya 59 Majimaji walifanya mabadiliko ya kumtoa Peter Mapunda na nafasi ikachukuliwa na Paulo Mahona ambaye aliongeza nguvu katika eneo la kiungo.

Dakika tatu baadae Mudathir tena aliipatia Azam goli la pili baada ya kazi nzuri ya Hamisi Mcha upande wa kulia na kumkuta mfungaji aliyefanya kazi nyepesi kuutumbukiza mpira wavuni.

Dakika ya 68 Majimaji walifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Luka Kikoti na kumuingiza Iddi Kipagwile na Azam akatoka Gadiel Michael na nafasi yake ikachukuliwa na Abdallah Kheri.

Azam ambao wameshatinga Fainali ya kombe la FA baada ya kuwaondoa Mwadui wamefikisha alama 58 katika mechi 25 walizoshuka dimbani na wanakamata nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Post a Comment

 
Top