BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
KUELEKEA mechi ya ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Simba siku ya Jumapili, timu ya Azam imeshusha pumzi baada ya nyota wake kadhaa waliokuwa nje ya kikosi kurejea uwanjani tayari kwa mtanange huo.

Mshambuliaji Kipre Tchetche na beki Pascal Wawa waliokuwa majeruhi wameanza mazoezi na wenzao huku kiungo Himid Mao akimaliza kutumikia adhabu yake baada kuoneshwa kadi tatu za njano kwenye mechi tatu mfululizo na sasa yuko huru kuitetea Azam.


Afisa habari wa klabu hiyo Jaffar Iddi Maganga alisema wachezaji watakao kosekana ni Shomari Kapombe ambaye anaendelea na matibabu huku Faridi Musa akiendelea na majaribio yake nchini Hispania."Tunamshukuru Mungu wachezaji wetu muhimu watatu wamerejea kikosini na wote wamefanya mazoezi ya pamoja asubuhi. Kwa sasa chaguo ni la mwalimu kupanga nani aanze kikosini, tunaowakosa ni Kapombe na Farid tu " alisema Jaffar.


Msemaji huyo pia alitanabaisha kuwa mchezo wao utakuwa mgumu kwavile timu zote zipo kwenye mbio za ubingwa kwahiyo kila moja inahitaji alama tatu ambazo ni muhimu kwa ajili ya kuendelea mbio hizo.


Azam tayari wametinga fainali ya kombe la FA na watacheza dhidi ya Yanga huku wakishika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu wakiwa na alama 58 baada ya kuteremka dimbani mara 25.

Post a Comment

 
Top