BOIPLUS SPORTS BLOG

NA Zainabu Rajabu, Dar
AZAM FC, wameandaa silaha na mbinu za kiufundi ambazo watatumia kuwamaliza wapinzani wao Mwadui FA kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA, itakayichezwa keshokutwa Jumapili, Uwanja wa CM Kirumba jijini Mwanza.

Azam imetua leo Ijumaa alasiri kutoka Tunisia ambako ilikwenda kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo imetolewa na Esperence kwa kufungwa bao 3-0 wakati mechi ya awali Azam ilishinda bao 2-1.

Msemaji wa klabu hiyo, Jaffar Idd alisema kuwa wanakwenda Kanda ya Ziwa ambako watakutana na mechi ngumu lakini tayari kocha wao Stewart Hall ameandaa mipango ya ufundi ambayo ni ya ushindi ili kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali.

“Mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa timu ya Mwadui lakini tayari kocha ameshandaa mbinu za kimchezo zitakazotupa ushindi na kusonga mbele kwenye michuano hii mikubwa ambayo itatupa nafasi ya kuiwakilisha nchi tena Afrika.

''Wachezaji wetu wamechoka na safari ndefu ya Tunisia ila haiwezi kusababisha kupoteza mechi hiyo kwani tayari akili zimehamia kwenye mechi ya kombe hilo, tutapambana kwa lengo la kupigania timu yetu itwae ubingwa huo wa FA pamoja na ligi,'' alisema Jaffar.

Wachezaji Kipre Tchetche na Pascal Wawa ambao walikuwa majeruhi na kukosa mechi ya kimataifa wanatarajia kucheza mechi hiyo kwani hali zao sasa zipo imara huku ikiendelea kumkosa Shomari Kapombe atakayekosa mechi zote za ligi zilizobaki pamoja na Farid Musa aliyekwenda kwenye majaribio nchini Hispania katika klabu za Union Deportiva Las Palmas na Athletic.

Post a Comment

 
Top