BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Chamazi


WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la shirikisho Azam FC wameutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuichapa Esparance ya Tunisia magoli 2-1 katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Azam waliuanza mpira kwa kasi na kucheza mipira mingi ya juu ambayo ilidhibitiwa vizuri na Esparance kutokana na wachezaji wao kuwa warefu, dakika ya 23 Ramadhani Singano na Faridi Musa waligongeana vizuri na kumwachia John Bocco ambaye lakini shuti lake lilitoka pembeni mwa goli.

Timu ya Esparance ndio walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa dakika ya 33 na Haithem Jouini kwa kichwa baada ya mabeki wa Azam kuzembea mpira wa krosi golini kwao. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko ya kumtoa Michael Balou na kumuingiza Frank Domayo ambaye alisaidia kwa kiasi kikubwa kupeleka mashambulizi mbele na kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo la Azam.

Dakika ya 48 John Bocco almanusura aisawazishie Azam baada ya kupiga kichwa ambacho kilitoka pembeni akiwa amebaki na kipa.

Baada ya kuwa wanaongoza kwa goli  moja wachezaji wa Esparance walianza kuchelewesha muda kitu kilichopelekea mwamuzi kuwaonesha kadi tatu za njano wachezaji wao.

Dakika ya 78 Faridi Musa aliisawazishia Azam baada ya kufanya kazi ya ziada kukimbia na mpira kutoka upande wa kushoto wa uwanja na kupiga shuti lililomshinda mlinda mlango wa Esparance Moez Ben Cherifia.

Dakika moja baadae Ramadhani Singano 'Messi' aliwapatia goli la ushindi Azam baada ya kupasiana vizuri na Farid na kuwachanganya mabeki wa Esparance kabla hajafunga goli safi.

Azam sasa wamepiga hatua moja mbele baada ya ushindi huu huku wakisubiri mechi ya marudiano itakayofanyika Aprili 20 jijini Tunis.

Mechi hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari Vijana Sanaa na wasanii Nape Nnauye na Wazuri wa Mazingira Mwigulu Nchemba.

Post a Comment

 
Top