BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma
MABINGWA wa kombe la Kagame timu ya Azam FC imetolewa kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-0 dhidi ya Esparance ya Tunisia.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Azam wakishambulia kwa umakini ili kupata goli la mapema ambalo lingewachanganya wenyeji wao lakini golikipa Aishi Manula nae kwa upande wake alikuwa makini kwa kuokoa michomo mikali toka kwa washambuliaji wa Esparance.

Pamoja na mashambulizi mengi kipindi cha kwanza lakini hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo shambulizi la kwanza langoni kwa Azam lilisababisha goli ambapo Idris Mhirsi alipiga mpira wa adhabu ulioenda moja kwa moja langoni baada ya mchezaji mmoja wa Esparance kufanyiwa madhambi mita chache kutoka golini.

Baada ya goli hilo Esparance waliendelea kuliandama lango la Azam huku golikipa Aishi Manula akifanya kazi ya ziada lakini dakika 63 alitoka bila kuwasiliana na walinzi wake na kusababisha Isama Sapili kuwapitia wenyeji goli la pili.

Azam ilifanya mabadiliko ya kumtoa  Farid Musa kuingia Mcha Hamis Vialli na Aboubakar Salum nafasi yake kuchuliwa na Himidi Mao na Didier Kavumbagu alichukua nafasi ya Waziri Salum lakini bado wana ramba ramba hao waliendelea kushambuliwa na Esparance.

Dakika ya 81 Ilyes Jelassi aliipatia goli la tatu Esparance baada ya mabeki wa Azam kushindwa kuokoa mpira langoni mwao.

Huu ni mwaka wa tatu Azam wanashiriki michuano ya kimataifa lakini wameshindwa kufika hatua ya robo fainali.

Post a Comment

 
Top