BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
MKATABA wa kiungo wa Ndanda FC, William Lucian 'Gallas' unamalizika mwishoni mwa msimu na yeye anataka kutimka lakini kocha wake, Hamis Malale amegoma kabisa na kwamba atahakikisha wanampa mkataba mpya.

Gallas alisaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya kutemwa Simba msimu uliopita na kutamka kuwa kwasasa anachoangalia ni ubora wa timu na masilahi mazuri kwake ndiyo atasaini mkataba.

Gallas alisema kuwa amejifunza mambo mengi ndani ya kikosi hicho na kikubwa ni kwamba wachezaji wa timu ndogo wanakuwa na ushirikiano mkubwa, hakuna anayekuwa juu ya mwenzake kama staa wa timu kama ilivyo kwa timu nyingine kubwa kama Simba, Yanga.

"Msimu ukimalizika nami mkataba wangu utakuwa umekwisha, nina asilimia chache sana za kubaki Ndanda na asilimia kubwa naangalia sehemu nyingine, naangalia ubora wa timu na masilahi mazuri nitakayopewa, kama Ndanda watanipa pesa nzuri naweza kubaki," alisema Gallas.

Kwa upande wa kocha Malale alisema: "Najivunia kuwa na mchezaji kama Gallas, najuwa wengi wanamtazama kwa mtazamo wa nje wa uwanja, akiwa nje ya uwanja unaweza kudhani ni mchezaji asiyekuwa na uwezo wowote uwanjani ila yupo tofauti sana na wachezaji wengine, anajituma mazoezi na kwenye mechi ni mpambanaji.

"Mchezaji kama huyo si rahisi kumwachia tu ili aondoke, nitakaa naye ili tuzungumze tuone jinsi gani ya kumpa mkataba mpya kwa makubaliano mapya, Gallas ameisaidia timu kwa kiasi kikubwa, si huyo tu wapo wengi ambao mikataba yao inamaliziaka ila tunaifanyia kazi," alisema Malale.

Tayari Ndanda imejihakikishia kubaki kwenye ligi mzimu ujao baada ya kukusanya pointi 33 na ina michezo mitatu mkononi, miwili nyumbani na mmoja ugenini.

Post a Comment

 
Top