BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
KESI ya beki wa Simba, Abdi Banda imeisha na sasa ametakiwa kurejea kikosini Jumatatu baada ya mechi yao na Toto Africans ya Mwanza itakayochezwa keshokutwa Jumapili.

Banda alisimamishwa kwenye kikosi hicho kwa kosa la utovu wa nidhamu baada ya kumgomea kocha wake Jackson Mayanja wakati timu hiyo ikicheza na Coastal Union. Mayanja alimtaka beki huyo kupasha ili  achukuwe nafasi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala' ikiwa ni dakika ya saba tangu mchezo uanze.

Habari zaidi zinasema kuwa beki huyo aliandika barua ya kujieleza juu ya kosa lake hilo ambalo sasa amesamehewa na huenda mazoezi akaanza Jumatatu ijayo.

Mayanja pia amekiri kwamba kwasasa hakuna tatizo tena na mchezaji huyo kwani suala lake lilikuwa linashughulikiwa na viongozi wake ambao bado hawajatangaza rasmi kufuta kwa adhabu hiyo ya kusimamishwa.

Meneja wa mchezaji huyo Abdul Bosnia alisema "Nimepata taarifa kutoka kwa kiongozi mmoja wa Simba kuwa tayari wamemsamehe ila mazoezi ataanza wiki ijayo. Nafikiri wametumia busara kumsikiliza maelezo yake na kumsamehe,"

Mayanja amekuwa kocha mwenye kusimamia nidhamu ambapo tayari alitoa adhabu kama hiyo kwa beki mwingine Hassan Isihaka na baadaye alimsamehe huku Hamisi Kiiza akipewa onyo.

Post a Comment

 
Top