BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
GOLIKIPA chaguo la kwanza wa Yanga, Ally Mustapha 'Barthez' ameanza mazoezi mepesi hii leo baada ya kuumia kwenye mchezo wa klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Al Ahly wiki iliyopita katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Meneja wa timu hiyo Hafidh Salehe amesema mchezaji huyo anaendelea vizuri na ameanza mazoezi mepesi ya peke yake leo kabla hajajiunga na wenzake katika siku zijazo.

" Barthez anaendelea vizuri na ameanza mazoezi mepesi leo ni matumaini yetu atarejea uwanjani muda si mrefu," alisema Hafidh.

Kwa upande wake daktari wa timu hiyo Edward Bavu amesema uchunguzi waliomfanyia golikipa huyo umeonesha hakuwa ameumia sana ni mshituko hasa baada ya kuanguka.

"Anaweza akakosa mechi ya Jumamosi dhidi ya Mtibwa au akajumuishwa kwenye kikosi inategemea ataamkaje siku hiyo lakini kwa sasa anaendelea vizuri," alisema Bavu.

Tayari Barthez ameshakosa mchezo mmoja wa ligi kuu dhidi ya Mwadui ambapo mabingwa hao waliibuka na ushindi wa magoli 2-1.

Yanga itasafiri wiki ijayo kwenda nchini Misri kwa ajili ya mechi ya marudiano na Al Ahly Aprili 19.

Post a Comment

 
Top