BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar

MWADUI FC jana ilifungwa na Yanga, matokeo ambayo yaliwafanya wabaki na pointi zile zile 34 huku baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wakionyesha kukata tamaa na matokeo hayo lakini mkongwe wa timu hiyo Athuman Idd 'Chuji' amewaambia kwamba kufungwa na Yanga kusiwarudishe nyuma.

Chuji alisema kuwa kilichopo sasa ni kujipanga kuhakikisha mechi zijazo wanashinda na kufikia malengo waliyojiwekea huku wakihakikisha wanashinda pia mechi ya Kombe la FA dhidi ya Azam ambayo itachezwa mjini Shinyanga.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars bado anaamini kiwango chao kuwa ni kizuri ila walishindwa kutumia nafasi walizozipata kwenye mechi hiyo ambapo wapinzani wao waliwawahi na kupata ushindi.

"Hizi timu zina wachezaji wenye umri mdogo, ambapo wakifungwa hukata tamaa ila kikubwa hapa ni kujipanga na kuangalia mechi zijazo tunafanyaje kupata ushindi, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri mechi zijazo, hivyo kufungwa na Yanga kusitukatishe tamaa, kikubwa tutambue kuwa tunahitaji kumaliza ligi tukiwa kwenye nafasi nzuri," alisema Chuji

Post a Comment

 
Top