BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma, Dar
MABINGWA wa zamani wa ligi kuu Tanzania bara Coastal Union 'Wagosi wa kaya' wamefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya kombe la FA baada ya kuwatoa Simba kwa magoli 2-1.

Simba iliingia uwanjani ikijiamini na kutengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza lakini walishindwa kuzitumia na dakika ya 19 Yusuph Sabo aliipatia Coastal  goli la kuongoza kwa kuunganisha mpira wa adhabu baada ya beki Emery Nimuboma kufanya madhambi.

Mpaka timu hizo zinaenda mapumziko Coastal walikuwa mbele kwa goli moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko ya kumtoa Said Ndemla na Justice Majabvi nafasi zao zikichukuliwa na Hamisi Kiiza na Awadhi Juma, mabadiliko hayo yaliongeza kasi kitu kilichopekea Simba kupata goli la kusawazisha kupitia Kiiza dakika ya 51 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mohammed Hussein.

Baada ya kupata goli hilo Simba waliendelea kutengeneza nafasi na kushambulia kwa kasi huku Coastal wakijilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza.

Dakika ya 61 kiungo wa Simba Awadhi Juma alipiga shuti kali la chini chini lililogonga mwamba na kurudi uwanjani.

Coastal waliendelea kulisakama lango la Simba kwa kushtukiza na dakika ya 85 mshambuliaji Ali Ahmed Shiboli aliangushwa kwenye eneo la hatari na beki Novaty Lufunga ambaye alioneshwa kadi nyekundu kutokana kuwa mchezaji wa mwisho kwa mujibu wa sheria 17 za soka.

Penati hiyo ilipigwa na Sabo aliyeipatia Coastal goli la ushindi na kuwapa nafasi wagosi hao kuingia nusu fainali.

Mpaka sasa timu nne tayari zimeingia nafasi ya nusu fainali ambazo ni Yanga, Azam, Mwadui na Coastal Union.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la mpira Tanzania TFF droo ya nusu fainali itapangwa kesho  jumanne sasa tatu usiku na itarushwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV

Post a Comment

 
Top