BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
MSHAMBULIAJI wa Toto Africans, Edward Christopher 'Edo' leo aliumizwa mbavu na beki wa Simba Hassan Kessy lakini amefafanua kuwa hana ugomvi wowote na mchezaji huyo kwani ni marafiki wakubwa tangu wakiwa Morogoro.

Kessy alimgonga ubavuni mshambuliaji huyo katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Simba ilifungwa bao 1-0 huku Kessy akipewa kadi nyekundu kwa kosa hilo.

Rafu hiyo ilitokea kipindi cha pili cha mchezo huo ambapo Edo alitolewa nje huku wengi wakidhani kwamba amezimia lakini ameweka wazi kuwa hakupoteza fahamu ila kifua tu kilibana kutokana na maumivu hayo.

"Katika mpira kuna vitu kama hivyo huwa vinatokea, mara nyingi inakuwa ni ubabe tu wa uwanjani ili kila mmoja amshinde mpinzani wake ndivyo ilivyotokea kwa Kessy na siwezi kusema kama amefanya makusudi naamini ni bahati mbaya tu.

''Nilijikuta tu nipo chini, sikupoteza fahamu bali kifua tu ndo kilikuwa kimebana sana na kusikia maumivu makali, kama alifanya makusudi nimemsamehe kwani yule ni mdogo wangu.

"Niliingia kucheza ila baadaye nilishindwa kutokana na maumivu makali niliyokuwa naendelea kuyasikia ndiyo maana niliomba kutoka nje. Ila mashabiki watambue kwamba Kessy ni rafiki yangu na wala siwezi kumchukia kwa hili," alisema Edo.

Akizungumzia mechi hiyo alisema "Ilikuwa ngumu kwa pande zote mbili ila tuliamini kwamba kama hatujapata ushindi basi tutapata sare, tunashukuru tumeshinda na kufikisha pointi 30, Simba hawakuwa na mbinu nyingine ya kutufunga kwani tuliwasoma tangu mechi ya mzunguko wa kwanza tuliyotoka sare." 

Simba imepoteza mechi hiyo na imebaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 wakati Yanga wapo kileleni kwa pointi 59, Azam wanashika nafasi ya tatu wakikusanya pointi 55.

Post a Comment

 
Top