BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
WINGA wa Azam, Farid Musa ambaye yupo nchini Hispania kufanya majaribio amewataja wachezaji wenzake Ramadhan Singano, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shiza Kichuya kuwa wana nafasi ya kucheza soka la kulipwa.

Mbali na hao Farid amewataja pia Kelvin Friday na Mudathir Yahaya ambao wote wanacheza Azam kuwa nao wakipata nafasi ya kucheza soka la kulipwa wanaweza kufanya makubwa.

Akizungumza na BOIPLUS kutoka Hispania, Farid alisema kuwa anaamini atafanikiwa katika majaribio yake kwani ana kasi, nguvu na uwezo wa kutengeneza nafasi za magoli.

''Naamini wamevutiwa na vitu vingi kutoka kwangu hivyo najiamini pia kuwa nitafanikiwa katika majaribio yangu, ukijiamini sidhani kama kuna kitu kinashindikana.

''Kujitambua kwangu ndiko kumenifikisha hapa namshukuru pia bosi wangu. Ila naaamini kuna wachezaji wengi Tanzania wanaweza kucheza soka la kulipwa kama Messi, Kichuya, Tshabalala, Kelvin na Mudathir,'' alisema Farid

Akizungumzia usumbufu anaoupata kutokana na umaarufu wake alisema: ''Jina kuwa kubwa haliwezi kunikatiza njiani kwasababu najielewa nataka nini na malengo yangu ni nini, ukijuwa malengo yako basi huwezi kuanguka.

''Nina ndoto ya kuifanya Tanzania nayo ijulikane kuwa ina wachezaji wazuri nashukuru pia Azam kwani ina maisha mazuri na rahisi ukilinganisha na timu nyingine japokuwa sijawahi kuzichezea zaidi ya kukutana na wachezaji mbalimbali kwenye timu ya Taifa na kusikia jinsi wanavyolalamika maisha magumu ya timu zao,'' alisema Farid.

Farid alisema kuwa huu ni muda muafaka kwake wa kucheza soka la kulipwa ambao alikuwa akiusubiri kwa kipindi kirefu. Farid atakuwa Hispania kwa muda wa mwezi mzima akifanya majaribio katika klabu za La Palmas na Atletic Bilbao.

Post a Comment

 
Top