BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe amewahurumia mashabiki na wanachama wa timu hiyo walio mvamia na kumletea fujo baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Toto Afrika ambao uliisha kwa Simba kulala goli 1-0.

 Baada ya kumalizika kwa mchezo huo mashabiki na wanachama wa timu hiyo walikusanyika kwenye gari la mwenyekiti huyo na kuanza kumtolea maneno machafu huku wakisema umefika muda wa viongozi wa timu hiyo kujiuzulu nyadhifa zao na kurudisha timu kwa wanachama kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata ndani ya wiki moja.

"Nawashangaa na kuwahurumia sana hawa mashabiki wananifuata mimi ambaye sio kocha wala mchezaji kosa langu liko wapi, wakati mwingine inabidi kabla hujafanya jambo lichunguze kwanza sio kukurupuka," alisema Hanspope.

Akizungumzia kuhusu kupoteza mechi mbili ndani ya juma moja Poppe alisema kuna vitendo vya rushwa kwa waamuzi ndivyo vimesababisha timu hiyo kupoteza mechi huku akiamini vinafanywa na watu wasioitakia mema klabu hiyo kwa maslahi yao binafsi.

"Ukiangalia katika mechi zote mbili tumecheza pungufu baada ya wachezaji wetu kuoneshwa kadi nyekundu tena kwa makosa ya kawaida."

"Angalia mechi ya jana Ibrahim Ajib alikuwa anavutwa jezi na mchezaji wa Toto na alikuwa kashamuacha nyuma lakini mwamuzi alionesha faulo kwetu na mchezaji wetu alioneshwa kadi ya njano," alisema Poppe .

Kama Simba itashindwa kuchukua taji la ubingwa msimu huu itakuwa haijashiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo.

Post a Comment

 
Top