BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Abra David Jr na Karim Boimanda
REAL Madrid jana imepewa kipigo cha mabao 2-0 ilipopambana na Wolfsburg katika mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya huko nchini Ujerumani, matokeo ambayo yameiweka mahali pagumu kufuzu hatua ya nusu fainali. 

Haya yamekuwa matokeo ambayo hayakutarajiwa na watu wengi hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo imetoka kuifunga Barcelona mabao 2-1 kwenye uwanja wao wa nyumbani tena wakicheza kandanda safi la mipango. Katika makala hii wachambuzi wa BOIPLUS wanaelezea mambo kadhaa yaliyomfelisha kocha wa Madrid Zinedine Zidane.


1. Uchezaji wa mabeki wa pembeni (Danilo na Marcelo)
 Tangu Zidane akabidhiwe timu hiyo amekuwa akiwaagiza mabeki wa pembeni wacheze katika mtindo wa kuingia katikati ya uwanja kusaidia ulinzi na wakati mwingine kuanzisha mashambulizi. Hii imempa mafanikio katika michezo mingi tu lakini hakupaswa kuitumia jana katika mchezo dhidi ya Wolfsburg ambao wanafahamika kwa mpira wa kasi na mawinga wajanja.

Kwavile mfumo huo unaotumiwa na Zidane hutoa nafasi wazi kwenye maeneo ya pembeni basi wapinzani walitumia mwanya huo kupiga krosi wakiwa huru na wakati mwingine kuingia ndani na kufanya mashambulizi. Mfumo huu utamsaidia kwenye mechi ya marudiano kwavile Wajerumani hao hawatafunguka sana kushambulia kwa kujivunia mabao mawili waliyonayo.

2. Casemiro hakuhitajika
Unapopambana na timu yenye kasi kama Wolfsburg hasa ikiwa nyumbani kwao huitaji kuwa na kiungo mkabaji kama Casemiro 'Combative Midfielder', badala yake Zidane  alihitaji viungo wabunifu tu kama Isco au James Rodrigues ambao wangesaidia kutengeneza mashambulizi bora.

Casemiro alikuwa nyota wa mchezo dhidi ya Barcelona kwavile timu hiyo hufanya mipango yake yote kupitia eneo la kati wakijivunia umahiri wa viungo wao kama Andres Iniesta, Ivan Rakitic na Sergio Busquet. Yeye alikuwa ametulia anasubiri kutibua mipango yao, hali ambayo ni tofauti kabisa na mchezo wa jana ambapo wajerumani hao walikuwa hawatabiriki kutokana na kasi yao.

Uwepo wa Casemiro uliinyima Madrid ubinifu hali iliyopelekea washindwe kutengeneza nafasi nzuri za mabao. Kama mmoja kati ya Isco au James angesimama nyuma ya BBC (Benzema, Bale na Cristiano) basi Wolfsburg wangepata wakati mgumu wa kutafuta ushindi huku wakiwa wanashambuliwa kwa mipango.

3. Mawinga walikariri mfumo
Wolfsburg walijua wanaenda kupambana na Madrid ambayo inasifika kwa mawinga wenye kasi duniani (Ronaldo na Bale), walichokifanya ni kuhakikisha mabeki wao wa pembeni hawapandi mara kwa mara, walibakia kuweka ulinzi madhubuti.

Kosa lililofanywa na Madrid ni kitendo cha Bale na Ronaldo kuendelea kushambulia  kupitia pembeni badala ya kubadili mpango na kuingia kati ambapo palikuwa na unafuu. Matokeo yake walikuwa wakiishia kupoteza mipira mara kwa mara.

Mchezo wa marudiano ndio utatoa majibu
Ukiingia kama mgeni kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu jiandae kushambuliwa kama nyuki. Madrid hutumia mabeki wa pembeni kupandisha mashambulizi na kupiga krosi huku mawinga wakiingia ndani kuongeza idadi ya washambuliaji. Kuwazuia hawa jamaa wasipate bao pale ni kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu sana na si tu 'kupaki basi'.

Hatua ya kwanza ya kuwazuia Madrid wasicheze mpira wao ni kuzuia tu. Wolfsburg watapaswa kutofunguka hata kidogo kwavile kufanya hivyo ni kuwaonyesha Madrid njia za kupita kwa kasi yao. Lakini tatizo linakuja kwamba Madrid wana viungo wabunifu ambao hata wajerumani wakipaki basi bado mtu kama Isco au James anaweza kupenya kwa chenga zake na kuingia eneo la hatari.
Swali ni je, Zidane atapangaje kikosi chake?

Post a Comment

 
Top