BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Tanga

MECHI za nusu fainali za Kombe la FA kati ya Yanga na Coastal Union, Azam na Mwadui zote zimechezwa kwa zaidi ya dakika 90 baada ya mechi zote mbili kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mechi ya Azam ilichezwa Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga wakati mechi ya Yanga na Coastal imepigwa katika dimba la Mkwawani jijini Tanga, katika dakika za kawaida Azam ndiyo ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu kupitia kwa mchezaji wake Hamis Mcha huku Hassan Kabunda akiisawazishia timu yake ya Mwadui.

Baada ya kuongezwa muda wa nyongeza wa dakika 30, Azam iliiongeza bao la pili mfungaji akiwa ni Mcha bao ambalo lilisawazishwa na Jabir Aziz kwa mkwaju wa penalti na kuzifanya timu hizo kumaliza mechi kwa dakika 120 ikiwa sare ya bao 2-2. Hivyo mechi hiyo ililazimika kwenda hatua ya matuta ambapo Azam ilishinda kwa penalti 5-3 ambazo ziliifanya timu hiyo kutinga hatua ya fainali ya FA.

Uwanja wa Mkwakwani, mechi ya Yanga ilishindwa kuendelea baada ya Amissi Tambwe aliyeingia kuchukuwa nafasi ya Donald Ngoma aliyeifungia Yanga bao la kwanza akisawazisha bao la Coastal Union ambao walianza kuona lango la wapinzani wao kupitia Youssouf Sabo aliyepiga shuti lililomshinda kipa Deogratius Munishi 'Dida'.

Bao la kwanza la Yanga lililalamikiwa na wachezaji wa Coastal pamoja na mashabiki wao kwamba ilikuwa ni la kuotea lakini mwamuzi Abdallah Kabunzi aliamuru mpira upelekwe kati kuashiria kwamba lilikuwa goli sahihi huku bao la Tambwe nalo likilalamikiwa kuwa halikuwa sahihi.

Baadaya bao hilo lililofungwa dakika ya 102, mashabiki waliosadikika kuwa ni wa Coastal Union walianza kufanya fujo kwa kurusha chupa za maji na mawe na kulazimika Kamisaa wa mchezo huo Osuri Kosuri kuamua kuvunja pambano hilo zikiwa zimemalizika dakika 15 za dakika za nyongeza.

Kosuri alisema kuwa: "Nitapeleka taarifa mahala panapohusika ndio wataamua nini cha kufanya, maana mechi isingeweza kuendelea kutokanana furugu zilizojitokeza, nadhani mmeona hali halisi ilivyokuwa."

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mashindano, Jemedari Said alifafanua juu ya hilo: "Kila mashindano yana kanuni na sheria zake, kwanza tutasubiri taarifa ya kamisaa wa mchezo tutaangalia kanuni zinasemaje ndipo tutaamua kabla ya Mei 25 ambapo fainali zinatakiwa zifanyike.

"Kwa hali ya kawaida taratibu na kanuni za mechi kuahirishwa na kuchezwa siku inayofuata huwa haisemi mechi ichezwe asubuhi kama zinavyochezwa hayo yanakuwa ni makubaliano tu, ila sheria inapaswa mechi ikishindwa kumalizika inatakiwa ichezwe kati ya saa 8 mchana hadi saa 4 usiku.

"Hii mechi imeshindwa kuendelea kuchezwa kwasababu ya vurugu, kama kuna vurugu ambazo ni hatari mechi hairudiwi ila mechi inaruhusiwa kuchezwa siku inayofuata kama ni sababu ya giza, mvua ama sababu nyingine inayohusiana na hayo, kikubwa ni kusubiri hiyo taarifa tutapeleka Kamati ya Mashindano kwa ajili ya kuijadili," alisema Jemedari.

Katika mechi hiyo ya Yanga, kocha Hans Pluijm alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Kelvin Yondani, Ngoma, Issoufou Boubacary nafasi zao zilichukuliwa na Malimi Busungu, Tambwe na Simon Msuva.

Mwamuzi Abdallah Kabunda alitoa kadi nyekundu kwa Adeyun Ahmed kwa kucheza rafu huku kadi za njano zikienda kwa Ally Ahmed, Ahmed Juma na Juma Mahadhi pamoja na beki wa Yanga, Oscar Joshua.

Kocha wa Coastal, Ally Jangalu ambaye alimtoa Ismail Mohammed na kumwingiza Ally Ahmed alisema kuwa "Waamuzi wetu hawatendi haki katika maamuzi, tumecheza vizuri lakini nafikiri wao walikuwa wanahitaji nani aingie fainali, hatuna cha kusema zaidi kwani ndiyo kama hivi imetokea,".


Mshika kidendera apigwa jiwe
Mwamuzi Charles Simon alipigwa jiwe na kumpasua kwenye paji la uso ingawa alipata huduma ya kwanza uwanjani hapo, ingawa alishindwa kuzungumzia lolote kwani hakuelewa nani alimpiga na jiwe hilo lililosadikiwa kuwa lilitoka kwa mashabiki hao.

Post a Comment

 
Top