BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar
KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) leo imemaliza kuwahoji viongozi wa timu ya Geita Gold Sport na Polisi Tabora kuhusu tuhuma ya upangaji wa matokeo kwenye mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) huku baadhi ya viongozi wakikacha kikao hicho muhimu.

Katika kesi hiyo timu zinazotuhumiwa ni nne ambazo ni Geita, Polisi, JKT Kanembwa na JKT Oljoro ambapo Polisi Tabora ilishinda bao 7-0 na Geita iliifunga Oljoro JKT. Hivyo hukumu hiyo inadaiwa ni ya kurasa 34 itasomwa kesho.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa baadhi ya watu waliohitajika kufika kuhojiwa hawakufika ambapo wengine walitoa taarifa ya udhuru kwa maandishi huku wengine hawakutoa taarifa yoyote.

Hata hivyo kutokuwepo kwa viongozi hao hakukuwazuia TFF chini ya kamati hiyo kuendelea na jukumu lao la kukamilisha mahojiano kwa wale waliofika na kuamua kutoa hukumu hiyo kesho Jumapili.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya TFF, Jerome Joseph Msami, akisema: "Kuna waliofika na wengine hawakufika, baadhi pia walitoa taarifa na wengine hawajatoa taarifa ila haikuzuiua lolote. Hukumu ina kurasa 34 za maandishi ambazo tutazisoma,"

Post a Comment

 
Top