BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
JANA mechi ya nusu fainali kati ya Coastal Union na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Mwakwakwani jijini Tanga haikumalizika katika muda wa dakika 30 za nyongeza lakini kiungo, Abdulrahiman Humud ametamka wazi kuwa hawakutendewa haki na kwamba hawana cha kufanya.

Katika dakika za kawaida za mechi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 ambapo Yanga iliongeza bao la pili dakika ya 102 lililofungwa Amissi Tambwe aliyechukuwa nafasi ya Donald Ngoma aliyefunga bao la kwanza wakati bao la Coastal lilifungwa na Yusuf Sabo.

Akizungumza na BOIPLUS, Humud ambaye alikuwa nahodha wa mechi hiyo alisema kuwa ingawa kikosi chao kina wachezaji wengi ambao hawana uzoefu lakini maamuzi yaliyokuwa yakitolewa hayakuwa sahihi kwao kwani yaliwaumiza.

"Tunakubali kwamba timu yetu haina wachezaji wengi wazoefu lakini tumecheza vizuri na tumefunga bao zuri, hebu angalia mabao yote ya Yanga yameamuliwa tu kuwa ni bao, ila Ngoma alikuwa ameotea na Tambwe alifunga kwa mkono, ila ndiyo hivyo hatuwezi kuamua lolote, watakachokiamua wao ndicho hicho hicho kitakachokuwa," alisema Humud

Baada ya mechi hiyo kuvunjika kutokana na vurugu za mashabiki wanaosadikiwa kuwa ni mashabiki wa Coastal Union, sasa kinachosubiriwa kumtangaza mpinzani wa Azam ni maamuzi ya Kamati ya Mashindano ambayo itapokea taarifa kutoka kwa msimamizi wa mechi hiyo, Osuri Kosuri itakayowasilishwa kabla ya fainali hizo zilizopangwa kufanyika mwezi ujao.

Tayari Azam wao walitinga hatua ya fainali baada ya kuifunga Mwadui FC kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 2-2 katika dakika 120 zilizochezwa. Ingawa kanuni na sheria za mashindano hayo ni kwamba timu itakayobainikiwa mashabiki wake kuanzisha vurugu basi ushindi unakwenda na timu pinzani.

Post a Comment

 
Top