BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Bakari Kagoma kwa msaada wa mitandao

MIAMBA ya soka nchini Hispania Barcelona na Real Madrid zinakutana katika mechi kubwa maarufu inayojulikana kama El Classico kwenye uwanja wa Nou Camp masaa machache yajayo.

Barcelona wataingia kwenye mechi hii wakiwa wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya mahasimu wao Real na katika mchezo wa mwisho Santiago Bernabeau wenyeji walifungwa magoli 4-0.

Katika mechi ya leo Real Madrid itakuwa na mastaa wake wote watatu wanaounda BBC Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo katika safu ya ushambuliaji huku Barca wakiwa na Lionel Mess, Luis Suarez na Neymar Jr kitu kinachochagiza utamu wa mechi hiyo.

Katika mechi za kimashindano zilizowakutanisha miamba hiyo Real Madrid imeshinda mara 92 huku Barca wakishinda mara 90 lakini katika michezo yote waliyokutana iwe ya mashindano au la Barcelona imeshinda Mara 109 Real imeshinda mara 96 pekee.

Tangu Ronaldo ajiunge na mabingwa hao wakihistoria akitokea Manchester united zimechezwa mechi 24 za El Classico Barca wameshinda mechi 12 Real 6 huku 6 zikitoka sare.

Messi ndiye anayeongoza kwa kufunga magoli katika mechi hizo baada ya kufunga magoli 21 na kusaidia upatikanaji wa magoli 10 huku Ronaldo akifunga magoli 15 na kusaidia magoli mawili

Real Madrid chini ya Zinedine Zidane wameshinda mechi nne mfululizo za la liga kitu ambacho kinaufanya mchezo wa leo kuwa mgumu kwa kila upande.

Barca chini ya Luis Enrique wameshinda mechi 22 za ligi kwenye uwanja wa Nou Camp na kufunga zaidi ya goli moja kila mechi.

Katika mechi baina ya miamba hiyo kadi nyekundu nne za mwisho walioneshwa wachezaji wa Real.

Kocha wa zamani wa Real Madrid Carlo Ancheloti anaipa nafasi Barca kuibuka na ushindi kwa kulinganisha mchezaji mmoja mmoja wa timu zote mbili na kusema wenyeji wataibuka kidedea usiku huu.

Kwa upande wake kocha wa sasa wa Real, Zidane ambaye ataiongoza  miamba hiyo kwa mara ya kwanza katika El Classico amesema ni muda wa wachezaji wa Real Madrid kulipa kisasi kwa Barca.

Post a Comment

 
Top