BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda

MSHAMBULIAJI hatari wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameifungia timu yake mabao matatu 'hattrick' katika ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Wolfsburg ya Ujerumani kwenye robo fainali ya UEFA iliyochezwa Santiago Bernabeu.

Madrid walioingia katika mchezo huo wakiwa nyuma kwa wastani wa mabao 2-0, walipata bao la kwanza katika dakika ya 16 kupitia kwa Ronaldo aliyemalizia krosi ya beki Danny Carvajal. Dakika moja baadaye mreno  huyo aliiandikia timu yake bao la pili kwa kichwa akiunganisha kona ya kiungo Toni Kroos.

Kipindi cha pili Madrid walionekana kulitafuta kwa nguvu bao la tatu ambalo ni la ushindi lakini Wolfsburg walionekana kujihami zaidi huku wakifanya mashambuli ya kushtukiza.


Dakika ya 77 Ronaldo aliwafungashia virago wajerumani hao baada ya kufunga bao safi kwa mkwaju wa adhabu ndogo uliopenya katikati ya ukuta wa mabeki na kuzitingisha nyavu.

Kwa ushindi huo, Madrid wameiondosha Wolfsburg kwa jumla ya mabao 3-2 .

Katika mchezo mwingine wa robo fainali usiku huu, Manchester City wameifunga PSG bao 1-0 hivyo kuwa wameitoa kwa jumla ya mabao 3-2 kufuatia sare ya mabao 2-2 waliyoipata kwenye mchezo wa awali nchini Ufaransa.

Post a Comment

 
Top