BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
KIRAKA wa Azam FC, Shomary Kapombe ametoboa siri ya uwezo wake wa kupachika mabao bora kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la FA kuwa ni mbinu anazopewa na kocha wake.

Kapombe amekuwa mchezaji mwenye bahati ya kuzifumania nyavu za wapinzani wake ambapo kwenye ligi tayari amefunga mabao nane sawa na straika wao John Bocco.

Kapombe ameendelea kupachika mabao kwenye Kombe la FA ambapo jana aliisaidia timu yake kupata ushindi mnono dhidi ya Prisons katika ushindi wa bao 3-1 yeye alifunga mawili.

Kapombe alisema kuwa kocha wake Stewart Hall amekuwa akimfundisha jinsi ya kucheza akitokea nyuma ya washambuliaji wake mfumo ambao unamfanya afunge zaidi kwani si rahisi kwa wapinzani wake kumkaba kutokana kwamba mawazo yao yanakuwa yakiwaza kuwakaba mastraika pekee.

"Huwa nafundishwa kucheza zaidi kwa kuwa nyuma ya mastraika hasa  nikitokea pembeni ni mfumo unaoniweka zaidi katika nafasi ya kufunga, tusipokuwa na mpira tunacheza kwa mfumo kama shepu ya mwezi tunakuwa watu watano tunalinda na tunaposhambulia tunakuwa wachezaji wanne katika eneo la adui.

"Mfumo huo unanipa nafasi kubwa ya kufunga kwasababu si rahisi kwa timu pinzani kunifikiria zaidi mimi maana natokea pembeni, wanakuwa wanawaangalia zaidi wale mastraika wawili wanaosimama pale kati na ndio sababu mimi nikiingia ghafla nakuwa huru," alisema na kuongeza

"Magoli yote kama la Toto, Yanga lililokataliwa na hata ya leo dhidi ya Prisons hakuna aliyewaza kuja kunizuia huwa natoka nyuma na kwenda kufunga inanipa muda mwingi kufika katika eneo kushambulia," alisema Kapombe

Kapombe alisema ni mbinu nyingi amekuwa anafundishwa na kocha wake lakini bado hajazifanyia kazi ipasavyo ila anaamini atafikia malengo ambayo kocha anahitaji.

"Ni rahisi kucheza kama winga. Stars tunacheza mfumo wa 4-4-2 hivyo  nikicheza namba mbili ni rahisi sana tofauti na tunavyocheza Azam nafanya kazi ngumu zaidi. Si mara ya kwanza kucheza kama winga na nilibadilika baadaye kucheza kama beki nikiwa Polisi Moro na hata timu Simba nilicheza nafasi hiyo," alisema

Post a Comment

 
Top