BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar

Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr akiwa na kocha wa sasa wa timu hiyo Jackson Mayanja kabla Kerr hajatimuliwa

KOCHA wa zamani wa Simba, Dylan Kerr ameipa nafasi kubwa timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kile alichodai kuwa alikiandaa kikosi hicho ambacho sasa kinafundishwa na Jackson Mayanja raia wa Uganda kutwaa ubingwa huo.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24 na kufuatiwa na Yanga yenye pointi 50 ikicheza mechi 21 huku Azam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 50 pia.

Matumaini ya Kerr ni kutokana kwamba wapinzani wao wana mechi ngumu za kimataifa ambapo Yanga inashiriki michuano ya Mabingwa wa Afrika na itacheza dhidi ya Al Ahly wakati Azam inashiriki Kombe la Shirikisho watacheza na Esperance ya Tunisia, mechi zote zitachezwa wikiendi ijayo jijini Dar es Salaam.

Kerr ambaye alikaa Simba kwa miezi sita, alisema kuwa kitu pekee anachojivunia akiwa Msimbazi ni msingi mzuri aliouacha ambao anaamini hadi sasa unaisaidia Simba ingawa amedai kuwa isingekuwa rahisi kukamilisha mipango yote kwa kipindi kifupi.

“Ukiangalia Yanga na Azam wana presha na mechi za kimataifa, ratiba imewabana hivyo ni fursa kwa Simba kufanya vizuri na kutwaa ubingwa huo. Naamini nafasi yao ni kubwa kuliko Yanga na Azam, dawa ni kujiamini na kuongeza juhudi tu," alisema Kerr

Simba ina nafasi ya kutwaa ubingwa endapo watashinda michezo yao sita iliyobaki na kuziombea Yanga na Azam zipoteze japo mechi moja katika  mechi zao zilizosalia. Timu hizo kila moja ina mechi tatu za viporo mkononi .

Post a Comment

 
Top